ADC: Tutashiriki uchaguzi wa marudio Zanzibar

Chama cha Allience for Democratic Change (ADC) kimesema kipo tayari kushiriki uchaguzi wa marudio kwa kadri itakavyopangwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec), mgombea urais kupitia chama hicho, Hamad Rashid Mohammed amesema.

Alisema hatua ya ADC kushiriki uchaguzi wa marudio ni sehemu ya kuendeleza mapambanao ya kutafuta demokrasia ya kweli.
Hatutagomea kwa maana kuugomea uchaguzi huo ni sawa na kumuachia nguruwe akala muhogo, tukakosa yote,  alisema Hamad.

Pia alipingana na ripoti za waangalizi wa kimataifa walioulezea uchaguzi huo wa Oktoba 25, mwaka huu, kwamba ulikuwa huru na haki.

Alisema waangalizi hao walijikita zaidi kuangalia uchaguzi huo upande wa Unguja kuliko Pemba hivyo kutoa mwanya wa kuwapo upotoshwaji kwenye ripoti zao.

Waangalizi wa uchaguzi kutoka nje ya nchi wamefanya upendeleo hawakufika kisiwani Pemba na zaidi walijikita Unguja, sasa nawashangaa wanaposema uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa huru na haki,î alisema.

Alisema ADC haina imani na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) na kwamba watendaji wake wanapaswa kujiuzulu.
Alisema muundo wa Zec umeshindwa kuifanya itekeleze majukumu yake na kusababisha vyama vilivyo na wajumbe ndani ya tume hiyo kuweka mbele maslahi ya kisiasa.

Zec imeshindwa kusimamia uchaguzi huu uliotarajiwa kuwa huru baada ya kuwapo Serikali ya Umoja wa Kitaifa, alisema.
Kwa upande wake, Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS), kimetoa hatua ya Mwenyekiti wa Zec kufuta uchaguzi huo haikubaliki kwa mujibu wa sheria na katiba ya Zanzibar.
Rais wa ZLS, Awadhi Ali Said aliitaka Zec kufuta tamko hilo na kuendelea kuhakiki matokeo ya majimbo 23 yaliyobaki, kisha kumtangaza mshindi halali.

Awadhi alimtaka Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein aunde tume ya kumchunguza Jeche dhidi ya madai ya kushindwa kufanyakazi zake na ikiwa itathibitika kukosa uadilifu, amfukuze kazi. Pia alipendekeza kuchunguzwa kwa waliomshinikiza Jeche kuyafuta matokeo ya uchaguzi huo na watakapobainika wachukuliwe hatua za kisheria.