Anna Mghwira amdai Magufuli Katiba mpya

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Anna Mghwira amemtaka Rais Mteule Dk John Magufuli kutekeleza utashi wa wananchi kwa kuwapatia Katiba mpya.

Mwenyekiti huyo, ambaye ameshika nafasi ya tatu katika mbio za urais wa Jamhuri ya Muungano, pia amemtaka Dk Magufuli kuhakikisha anadumisha umoja wa kitaifa na kuondoa umasikini, huku akimkabidhi ilani ya chama hicho ili aitumie katika kipindi chake cha uongozi.

Mghwira alisema hayo saa chache baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumkabidhi Dk Magufuli cheti cha kumtambua kuwa mshindi wa mbio za urais kwenye hafla fupi iliyofanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es salaam.

Mgombea huyo ni mwanamke pekee aliyejitosa kuwania nafasi ya urais katika uchaguzi wa mwaka huu, alimtaka Dk Magufuli kuanza na jambo lililokuwa likizungumzwa mara nyingi katika kampeni za Uchaguzi Mkuu ambalo ni mabadiliko.

Alisema miongoni mwa mambo yanayohitaji mabadiliko ya haraka katika uongozi wake ni kuwapatia wananchi katiba mpya, kudumisha umoja wa kitaifa na kuwaondolea wananchi umasikini kwa sababu Tanzania ina utajiri mkubwa.

Mghwira, ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa, alipewa nafasi hiyo ya kuzungumza kwa niaba ya wagombea urais wa mwaka huu. Wagombea waliohudhuria kwenye hafla hiyo walikuwa watano baada ya mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, aliyeshika nafasi ya pili, Hashim Rungwe (Chaumma) na Macmillan Lyimbo wa TLP, kutofika.

Awali kabla ya hafla hiyo, Mghwira aliliambia gazeti hili kuwa Tanzania ni tajiri lakini Watanzania wenye nchi yao wamebaki kuwa masikini, hivyo wananchi wamemchagua Dk Magufuli kwa sababu wana imani naye na hivyo anatakiwa kuhakikisha hawaendelei kuwa masikini, haki fikra.

“Umasikini walio nao Watanzania ni wa uongozi bora, nimekubali na nina imani Watanzania walio wengi wamekubali kuwa Dk Magufuli ndiyo Rais wa Awamu ya Tano,” alisema.

Wagombea wengine waliozungumza na Mwananchi walisisitiza kuwapo na amani, utulivu, kutatua kero tatu za wananchi ambazo zipo tangu nchi ipate uhuru ambazo ni ujinga, maradhi na umasikini.

Chifu Lutalosa Yemba, aliyewania urais kupitia ADC, alisema kuwa wakati wanaingia kwenye kinyang’anyiro hicho, alikuwa na lengo la kuondoa maadui hao watatu waliodumu kwa miaka mingi nchini. Hivyo Rais wa Awamu ya Tano ahakikishe anapambana na matatizo hayo.

Kuhusu kuwa nje ya Ukawa , Yemba alisema hakuingia huko kwa sababu hakuona kama atakuwa salama kwa sababu hakukuwa na msingi wa umoja huo, ingawa alisema hana tatizo na uwepo wake na hadhani kuwa vyama vilivyokuwa nje ya umoja huo vimesababisha wapinzani wasichukue nchi.

Alisema kutokana na uzoefu wake wa kugombea ubunge na urais, uchaguzi wa mwaka huu ulikuwa huru na wa haki.

Alisema hapo awali, hata kampeni zilikuwa na vitisho, ilikuwa ngumu kumtaja kiongozi mwingine jukwaani kwa kuhofia vitisho, lakini mwaka huu kila mgombea alikuwa huru kuzungumza, kuhoji anapoona hapajakaa sawa.

Lyimo, aliyegombea kwa tiketi ya TLP, alisema uchaguzi haukuwa huru na haki kwa sababu kuna dosari na kasoro nyingi huku wananchi wakilazimishwa kukubali na kuamini wanachotaka watu wachache.

Alisema kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar ni moja tu ya dosari nyingi zilizofumbiwa macho na matakwa ya watawala.

“Nimekubali matokeo na kushindwa kwa sababu ya kutetea haki za Watanzania walio wengi ambao hawataki vurugu, wanataka amani itawale. Tangu awali kulikuwa na harufu ya vurugu, sikutaka niwe chanzo cha vurugu hizo,” alisema Lyimo.

Janken Kasambala, aliyewania kiti hicho kupitia chama cha NRA, alisema uchaguzi umekwisha hivyo Watanzania waweke kando mambo ya siasa badala yake waungane kupambana kujenga nchi.

“Tuachane na masuala ya siasa, tufanye kazi, tuungane kujenga nchi, tuachane na tofauti za kisiasa, kwani tulikuwa tunatafuta mshindi mmoja atakayeiongoza nchi, na sasa amepatikana,” alisema Kasambala.

Fahmi Dovutwa wa UPDP alisema Watanzania warudi kama zamani waendeleze maisha na kuachana na ushabiki kisiasa.

uliokuwepo wakati wa kampeni kwa sababu Rais amepatikana.

Alisema hata waangalizi wa kimataifa hawana nafasi ya kuingilia masuala ya kisiasa ya ndani kwa sababu hata kwao huwa wanaharibu, hivyo wananchi, viongozi wasifanye maamuzi kwa kuwasikiliza wao badala yake waangalie mustakabali wa nchi na wananchi wake.