Davis Mosha atangaza kuachana na siasa

Aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo la Moshi Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Davis Mosha ametangaza rasmi kung’atuka katika siasa, akiwatuhumu viongozi wa mkoa wa chama hicho kuhujumu CCM.

Mosha aliangushwa katika kiti cha ubunge na Japhary Michael (Chadema) aliyeibuka kidedea kwa kupaa kura 51,646 dhidi ya kada huyo wa CCM aliyeambulia kura 26,920 katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Uamuzui huo uliibua vilio na simanzi katika  viwanja vya Penfold-Njoro vilivyoko katika Manispaa ya Moshi, ambako baadhi ya wanachama wa CCM walielekeza masikitiko yao kwa viongozi wa mkoa na wilaya kwamba ndio chanzo cha CCM kushindwa kukomboa jimbo hilo kwa miaka 20 sasa.  Kada huyo alifikia maamuzi hayo wakati akizungumza na waananchi katika mkutano wa hadhara ulifanyika katika viwanja vya relini mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, akiwa na  lengo la kuwashukuru na kuwaaga baada ya ushirikiano aliopata kutoka wa wananchi hao.

Mosha alisema kwa sasa haoni sababu ya kuendelea kujihusisha na siasa kutokana na kile alicho dai kuwa baadhi ya viongozi wa CCM mkoa wa kilimanjro kuwa ni ndumilakuwili na kwamba hawakuwa na lengo la kukombo jimbo la Moshi Mjini.

“Sitakaa kamwe katika maisha yangu mimi kujihusisha na siasa tena bali nitarudi na kuendelea na biashara zangu kwani viongozi wa CCM Moshi hawana lengo la kukombo jimbo bali wamekuwa walafi na wamekuwa wakiunga mkono CCM mchana, lakini usiku ni Ukawa,” alisema kwa masikitiko.

Aidha alisema haoni sababu ya kuendelea kuwadanganya wananchi wa Moshi kwamba ataendelea na siasa na haoni sababu ya kupinga au kukataa matokeo yaliompa ushindi mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Michael.

Aliendelea kusema kuwa iwapo viongozi wa (CCM) katika jimbo la Moshi Mjini hawatabadilika, jimbo hilo litaendelea kushikiliwa na upinzani kutoka na ukweli kwamba baadhi yao wamekuwa wakikihujumu chama hicho.

“Nawapenda sana watu wa Moshi nimekaa na nyie kwa zaidi ya miezi mitatu nimeacha familia yangu nimekuja kushirikiana na ninyi, sasa nawaahidi jambo moja tu kwamba ahadi zote nilizozitoa nitazitimiza kwa asilimia 100,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Moshi, Elizabeth Minde, alisema CCM kuanguka katika nafsi ya ubunge na viti vya udiwani ni kutokana na wananchi kutoelimishwa vya kutosha juu ya umuhimu wa kuchagua chama  hicho.