Katika umri wa
miaka 13, azaa na binti wa miaka 15
Wapata mtoto wa
kike, baba hajui hata bei ya nepi
MTOTO mwenye umri wa miaka 13, Alfie Patten, ndiye
anayetajwa kuwa baba mdogo zaidi duniani, akiwa amepata mtoto na binti wa umri
wa miaka 15, wote wakiwa raia wa Uingereza. Ingawa Alfie ana umri wa miaka 13
lakini ana umbile dogo ambalo kimtazamo anaweza kutafsiriwa kama mtoto wa miaka
minane.
Kwa mujibu wa habari iliyochapishwa katika gazeti la The
Sun, la nchini Uingereza Februari, mwaka jana, Alfie amepata mtoto na rafiki
yake wa kike aitwaye Chantelle Steadman.
Siku moja tu mara baada ya kupata mtoto, Alfie aliulizwa
kama anafahamu chochote kuhusu bei ya nepi, naye akajibu; “Nadhani ni gharama
kubwa sana, ingawa sijui vizuri mambo haya, sijui kama nitamudu gharama hizo.
Wakati mwingine baba yangu hunipa pauni 10 hivi za kutumia (zaidi ya Sh
20,000).”
Alipata mtoto huyo, waliyemwita kwa jina la Maisie, Februari
mwaka jana kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni matokeo ya kupinga vitendo
vya utoaji mimba miongoni mwa vijana.
Naye Chantelle amenukuliwa akizungumzia namna asivyopenda
kuingia katika rekodi ya utoaji mimba akisema; “nilidhani itakuwa vema
nikijifungua mtoto.
Alfie anatajwa kuwa na urefu wa futi nne na gazeti la The
Sun, lilimnukuu akizungumzia tukio hilo na hasa mwitikio wa familia yake.
Anasema: “Pindi mama yangu alipogundua suala hili, nilidhani nitakuwa kwenye
mgogoro. Mimi na mwenzangu tulitaka mtoto lakini tulihofia namna mwitikio wa
watu utakavyokuwa.
"Sikuwa nafahamu chochote kuhusu maana ya kuwa baba.
Nitakuwa mwema, na mwenye kujali."
Tukio hilo lilivuta hisia za wengi na kati ya hao ni
wanasiasa nchini Uingereza. Mfano, kiongozi wa chama cha Conservative, David
Cameron anazungumzia suala hilo akisema: "Nilipoona picha ya watoto hao
wazazi kwenye gazeti, nilianza kuwa na wasiwasi jinsi gani watoto wa enzi hizi
hapa Uingereza wameanza kuwa wazazi.
“Natumaini kwamba kwa kiasi fulani watoto hawa watakuwa
katika maadili kama wazazi wanaowajibika kifamilia, lakini ukweli ni kwamba
kuwa wazazi si suala ambalo walipaswa kuliwaza kwa umri wao."
Naye Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, alikataa kutoa
maoni yake kuhusu tukio hilo lakini akiweka bayana kwamba; “Jambo la muhimu ni
hatua zilizochukuliwa na serikali kuhakikisha hakuna mimba za utotoni.”
Baba wa Alfie, Dennis mwenye umri wa miaka 45, naye
alizungumzia hali hiyo akisema mwanawe hakuwa katika hali ya uelewa wa kutosha
muda mfupi kabla ya mwanawe kuzaliwa na kwamba alipozaliwa, mwanawe huyo
alikuwa na shauku kubwa ya kumbeba mtoto mikononi mwake.
Dennis alinukuliwa akisema: “Angeweza kubaki nyumbani
akiendelea na michezo yake kama mtoto, lakini alikuwa akijitahidi kufika
hospitalini karibu kila siku (baada ya ‘mkewe’ kufikishwa hospitalini kwa ajili
ya kujifungua).
Inaelezwa kuwa vijana hao walipeana ujauzito wa mtoto wao,
Maisie, baada ya kulala pamoja na kufanya ngono bila kutumia kinga. Waligundua
kuwa Chantelle amepata ujauzito baada ya ujauzito huo kufikia umri wa wiki 12,
yaani zaidi ya miezi mitatu.
Lakini licha ya kugundua hivyo, alifanya suala hilo la siri
hadi ujauzito huo ulipofikisha umri wa wiki sita, baada ya mama wa Chantelle,
Penny mwenye miaka 38, kuanza kutilia shaka mwenendo wa binti yake na hasa
baada ya kubaini kuwa uzito wake umekuwa ukiongezeka kinyume cha hali ya
kawaida.
Alfie, awali aliogopa kuwaeleza hata ndugu zake wa karibu
akihofia kuwa ‘stori’ yake ya kuwa baba ikifika shuleni basi anaweza kuwa
katika mazingira tata hususan kati yake na rafiki zake wanafunzi.
Chantelle alijifungua salama binti huyo katika Hospitali ya
Eastbourne, huko East Sussex, baada ya kulazwa hospitalini hapo kwa saa tano
akiwa katika chumba cha kujifungulia, maarufu kama labour. Baada ya kujifungua,
binti huyo alilieleza gazeti la The Sun kuwa; “Nimechoka, nilikuwa na wasiwasi
sana nikiwa labour lakini sasa nina furaha.”
Akisimulia jinsi yeye na mwanaume wake walivyobaini kuwa ana
ujazito, Chantelle alisema ni kutokana na maumivu ya tumbo aliyokuwa akiyahisi
na hivyo akiwa na mpenziwe walikwenda kupata ushauri wa daktari
Anasema: "Mimi na Alfie tulikwenda kumwona daktari na
baada ya kumweleza akatuuliza kama tumewahi kufanya mapenzi. Mimi nikajibu
ndiyo naye akatueleza ni lazima mimi nipimwe ujauzito. Alinipima na kunieleza
kuwa mimi ni mjamzito. Nilianza kulia na sikujua cha kufanya. Daktari
akanieleza ni lazima nimwambie mama yangu, lakini niliogopa kumwambia.
"Mimi na mwenzangu hatukufikiri kwamba tunahitaji
msaada wa wazazi wetu. Unajua ukiwa mjamzito huwezi kufikiria haraka haraka
kuwaeleza wazazi wako, kwa sababu akili inayojitokeza ni kwamba wataweza hata
kukuua kwa hasira."
Lakini mama yake binti huyo, Penny, alianza kuhisi mwanawe
hayuko katika hali ya kawaida mbali na kuongezeka uzito, aligundua kuwa fulana
mojawapo kati ya alizokuwa akivaa ilionyesha ‘kitumbo’ chake kujitokeza zaidi
ya kawaida.
Kwa upande mwingine, dada wa Alfie, amemlalamikia ndugu yake
huyo kutokana na kuwa mzazi katika umri mdogo zaidi, akisema huo ni uzembe wa
ovyo.
Dada yake huyo, Nicole mwenye umri wa miaka 19 hata hivyo
hakusita kuweka bayana kuwa anaelekeza tuhuma zake kwa baba yao mzazi, kwa
kuacha Alfie ampachike ujauzito Chantelle. “Kama si yeye (baba), basi Alfie
asingekuwa katika hali hii. Baba yao kwa sasa anaishi na mama wa kambo, Nicola.