Nyanya ni aina ya mboga inayo zalishwa kwa wingi sana duniani. Kwa
Tanzania, nyanya ni zao la kwanza katika mazao ya mboga linalo limwa na kuliwa
kwa wingi ukilinganisha na mboga zingine. Nyanya hutumika karibu Katika kila
mlo. Kulingana na umuhimu wa zao hili kama chakula na pia kama
zao linalomwingizia kipato Mkulima, kuna haja ya kutoa mafunzo kuhusu mbinu
bora za uzalishaji wake. Pia kuna umuhimu wa kufundisha wakulima kutoka sehemu
zingine wasiolima zao hili ili nao waweze kuzalisha nyanya na hivyo kuongeza
idadi ya aina za mboga katika maeneo yao.
MAHITAJI YA ZAO LA
NYANYA
Nyanya hustawi vizuri kwenye maeneo ya joto, yasiyo na
ukungu mwingi hasa wakati zao linatoa maua
na matunda. Zao hili hupenda kipindi kirefu cha jua na joto ili kuongeza ukuaji
wa matunda na kupunguza magonjwa ya aina ya ukungu/kuvu. Zao hili halipendi
mvua nyingi ingawa linahitaji maji kwa wingi. Katika kipindi chenye mvua nyingi
na jua kidogo nyanya hushindwa kutoa maua
na matunda ya kutosha bali huweka majani mengi. Katika kipindi hiki pia, nyanya
hushambuliwa sana
na magonjwa ya ukungu. Nyanya hupendelea udongo unaopitisha maji kwa urahisi na
wenye rutuba ya kutosha na hivyo hupenda samadi. Udongo uwe umetifuliwa vya
kutosha kuruhusu mizizi kushika vema.
AINA ZA NYANYA
Kuna aina kuu mbili za nyanya kulingana na ukuaji wa mmea:
yaani nyanya inayo refuka zenye kuhitaji egemezi (mfano Money maker) na aina ya
pili ni nyanya fupi zenye kutoa matawi mengi mfano Roma na Cal J.
UKUAJI WA MICHE
Miche ya nyanya huzalishwa kwenye kitalu kwa kupanda mbegu.
Mbegu za nyanya huota baada ya siku 5 hadi 10. Baada ya kukua kitaluni kwa muda
wa wiki 4 hadi 5 toka kuota kwa mbegu, miche hupandwa shambani. Kabla ya
kupandikiza shambani miche huandaliwa kwa kupunguza umwagiliaji maji kwa siku
moja au mbili ili miche izoee hali ngumu kabla ya kuhamishiwa shambani. Hapo
shambani miche hupandikizwa kwa kuzamishwa katika kina kirefu zaidi ya ilivyo
kuwa kitaluni.
Hii inasaidia miche kutoa mizizi ya pembeni mingi zaidi kwa
ajili ya kufyonza maji pamoja na virutubisho aridhini. Baada ya kupandikiza
mwagilia maji ya kutosha. Usimwagilie maji juu ya mche wa nyanya. Katika
kipindi cha jua kali, tandaza nyasi kwenye tuta ili kupunguza upotevu wa maji
na unaweza kuweka kivuli kwa kutumia majani ya miti au migomba. Kulingana na
aina ya nyanya na rutuba ya udongo, nafasi ya kupandia ni sm 60 kati ya mstari
hadi mstari na 45 hadi 60 nafasi ya mche hadi mche. Kama
udongo hauna rutuba ya kutosha inapendekezwa kutumia nafasi kubwa ya kupanda.
UTUNZAJI
Nyanya fupi zisizo refuka kwenda juu, ni rahisi sana kutunza na hazihitaji
huduma nyingi. Tatizo kubwa ni kuwa kwa kutambaa chini, katika kipindi cha mvua
huwa karibu na magonjwa yatokanayo na udongo. Katika kipindi cha jua kali,
matunda huungua kwani mmea huwa na majani machache tu yanayo kinga matunda
yasipigwe na mionzi ya jua.
MBOLEA
Licha ya mbolea ya kupandia, unashauriwa kuongeza mbolea
kipindi cha wiki mbili au tatu baada ya kupandikiza miche bustanini. Mbolea hii
ya kukuzia iwekwe kuzunguka shina la mmea kwa umbali wa sentimeta 5 hadi saba
kutoka kwenye shina. Kwa mbolea kama vile CAN,
NPK, au SA tumia kifuniko kimoja cha soda kwa shina. Mbolea hii inaweza kuwekwa
mara mbili kabla ya mvuno wa kwanza. Ili kurefusha kupindi cha uzaaji wa zao la
nyanya (na hata mazao mengine yatoayo matunda kama vile nyanya chungu,
biringanya, pilipili hoho, nk) inapaswa kuongezea mbolea katika kipindi cha
uvunaji mfano baada ya kuvuna mara mbili unashauriwa kuongeza mbolea ya samadi
na mbolea kama vile NPK.
Hii inasaidia mmea kuendelea kutoa maua bila kuchoka. Kwa kawaida nyanya fupi
jamii ya “Roma” huweza kuzaa na kuvunwa kwa kipindi cha wiki 6 hadi 8 tu.
Lakini kama utakuwa unaongezea mbolea na kukazania matunzo ya bustani (hasa
usafi wa bustani na Kumwagilia maji ya kutosha), nyanya zinaweza kuendelea
kuzaa kwa muda mrefu zaidi. Hii ni tofauti
na mazoea ya wakulima wengi kuwa mara nyanya zianzapo kuzaa
huduma za palizi na usafi wa shamba huachwa na kutilia maanani kazi ya kuvuna
pekee. Hii inajitokeza zaidi kwenye aina ya nyanya fupi.
Kwa nyanya fupi ni vizuri kuhakikisha kuna matawi mengi
iwezekanavyo ili kuweza kupata matunda mengi zaidi. Hivyo usipunguze matawi
katika aina hii ya nyanya. Kwa nyanya ndefu zenye kuhitaji egemezi,tunashauriwa
kukuza nyanya kwa tawi moja lisilo na vichipukizi pembeni au matawi mawili na
kuacha mnyanya urefuke.
Kupunguza majani ni muhimu pia katika kupunguza maambukizo
ya ukungu katika shina na pia kutoa nafasi ili
mwanga kupenya na kuruhusu mzunguko wa hewa. Majani yapunguzwe
kipindi cha asubuhi kwa kutumia mkono na siyo kisu kwani kinaweza kueneza
magonjwa kutoka mche hadi mche. Kwa nyanya ndefu, majani ya chini ya matunda
huondolewa kadiri unavyo endelea kuvuna. Unashauriwa upunguze majani wakati wa
asubuhi kwa kutumia mkono na pia usitoe zaidi ya majani matatu katika mmea kwa
mara moja.
UMWAGILIAJI
Nyanya ni zao linalohitaji maji mengi sana kwa ajili ya ukuaji wa mmea na matunda
yake. Umwagiliaji uwe wa kulingana kwa kila siku iliyo pangwa. Usibadilishe
ovyo kiasi cha maji na ratiba ya kumwagilia. Hii inasababisha kuoza kwa kitako
cha nyanya. Pia ili kutunza maji katika udongo, inashauriwa kuweka matandazo
katika mzunguko wa shina la nyanya au bustani yote. Nyanya inayo kua vizuri
hutumia maji lita mbili kwa siku
katika kipindi cha jua kali. Hivyo katika umwagiliaji ni
busara kuzingatia kiasi hiki cha maji katika kipindi kama
hiki. Pia kama unatumia keni, mpira au bomba
usimwagilie maji juu ya matawi ya nyanya kwani umwagiliaji wa namna hii
utasababisha kuenea kwa magonjwa ya ukungu.
MATATIZO YA KILIMO
CHA NYANYA
Matatizo yanayosumbua kilimo cha zao hili ni magonjwa na
wadudu waharibifu. Hapa tutajifunza mbinu mbali mbali za kuzuia magonjwa na
wadudu waharibifu.
WADUDU WAHARIBIFU
FUNZA WA NYANYA (Funza wa vitumba)
Huyu funza hushambulia mazao mengine kama
vile pamba, mahindi, mtama, maharage n.k. Mdudu huyu hushambulia matunda ya
nyanya kwa kutoboa na hivyo kuyafanya yapoteze soko kwasababu hayafai kuuzwa
katika soko na pia yanaweza kuoza wakati wa usafirishaji. Ili kuthibiti piga
dawa ya kuua wadudu kama vile thiodan, sevin
ya unga, karate, selecron, n.k. Muarobaini hutumika pia katika kupunguza
uharibifu wa mdudu huyu.
INZI WEUPE
Wadudu hawa huruka ruka kwenye shamba la nyanya na kukaa
chini ya majani. Mdudu huyu hueneza magonjwa ya virusi kama
vile “ukoma wa nyanya”. Usafi wa shamba na mazingira ya yake ni muhimu katika
kupunguza kuzaana kwa wadudu hawa. • Ili kuthibiti wadudu hawa kwenye bustani
ya mboga na pia katika maficho yao, piga dawa kama vile karate, cypermethrin mara kwa mara. • Panda
mimea mingine (kama vile tumbaku) inayo vutia
wadudu hawa kwenye maeneo ya bustani kisha piga dawa katika miche ya tumbaku
ili kuwaangamiza kwa wingi.
MINYOO
Mdudu huyu hukaa kwenye udongo wenye unyevu wa kutosha.
Huvamia mizizi ya nyanya na kuharibu mfumo wa usafirishaji maji na chakula
kwenye nyanya iliyo athirika. Uking'oa mche wa nyanya utaona vifundo kwenye
mizizi.
KUZUIA
Mbinu za kuthibiti ongezeko la wadudu hawa ni kuharibu hali
ya udongo inayo mfanya aishi na kuzaana. Mbinu hizi ni:
• Kulima shamba kwa kutifua baada ya kuvuna nyanya ili
udongo wa chini ukae juani na kukauka. Hii inasaidia kuangamiza wadudu hawa kwa
joto na ukosefu wa maji.
• Choma moto na kuteketeza mabaki ya nyanya baada ya kuvuna.
• kuzungusha aina ya zao la nyanya au jamii ya nyanya na
mazao mengine yasiyo vamiwa na adui huyu. Hii huwafanya minyoo wasipate hifadhi
na chakula kutoka kwenye mimea wanayo tumia kuishi na kuzaliana. Hivyo idadi yao kupungua katika
udongo.
• kabla ya kupanda zao weka samadi nyingi katika udongo
kwenye eneo lililo athiriwa na wadudu hawa kwani hawapendi udongo wenye samadi
nyingi.
• Panda manung'a nung'a (Tagetes spp) katika eneo
lililoathirika na minyoo hawa, mimea hii hutoa sumu ya aina fulani ambayo huathiri
ukuaji na kuzaliana kwa minyoo hawa.
MAGONJWA
Uchunguzi umeonyesha kuwa katika maeneo ya Kilombero na
Gairo, nyanya na mazao mengine jamii ya nyanya ndiyo hushambuliwa sana na magonjwa kuliko
mazao mengine ya mboga.
UKUNGU
Huu ni ugonjwa unaopenda hali ya unyevu mwingi hewani. Hivyo
hujitokeza zaidi wakati wa masika. Pia sehemu zenye umande mwingi wakati wa
usiku, ugonjwa huu hujitokeza hata wakati wa kiangazi.
DALILI ZAKE
Ugonjwa huu hushambulia shina, maua na matunda. Kuungua kwa majani kama vile yamechomwa na maji moto. Chini ya jani utaona
unga unga mweupe. Matunda pia hushambuliwa na ugonjwa huu na hugeuka kuwa meusi
na magumu.
KUZUIA
• Inabidi kuchanganya mbinu mbali mbali za kupambana na
ugonjwa huu.
• Kwanza ni usafi wa shamba
kwa jumla yaani hakikisha unaondoa magugu katika bustani.
• Tandaza nyasi juu ya matuta yaliyo pandwa nyanya.
• Ondoa majani yaliyo zeeka na yanayo onyesha dalili za
ugonjwa huu. katika kupunguza majani, hakikisha sehemu za chini ya mmea ni wazi
na kuna mzunguko mzuri wa hewa. Punguza majani katika mmea ili kupunguza umande
na ukungu kwenye mmea.
• Baada ya kupunguza majani na machipukizi hakikisha unatupa
mbali majani hayo na siyo kuyaacha kwenye tuta la bustani.
• Ondoa kabisa mmea ulio na dalili za ugonjwa huu
• Kupiga dawa katika kipindi cha mvua mara baada ya mvua
kubwa. Fanya hivyo mara moja au mara mbili kwa wiki kutegemea na wingi au
mfululizo wa mvua.
Unapoona jua limetoka piga dawa ili ugonjwa usijitokeze
tena. Baadhi ya madawa yanayofaa kukinga ugonjwa huu ni Dithane M45, Bravo,
Benlate , Ridomil, Topsin n.k. Kumbuka kuwa kila
mwaka madawa yenye nguvu zaidi hutengenezwa, hivyo uliza
watalaam walioko karibu nawe. Ingawa Blue Copper inauzwa kwa bei nafuu, nguvu
yake in kidogo sana
kuthibiti huu ugonjwa. Muarobaini pia unaweza kutumika kupunguza ugonjwa huu.
Changanya unga unaotokana na mbegu za muarobaini kiasi cha nusu kilo ya unga
katika lita 20 za maji.
UKOMA WA NYANYA
Huu ni ugonjwa wa virus unao enezwa na inzi mweupe. Inzi
hawa hushambulia zaidi nyanya wakati wa kiangazi, hasa kipindi cha joto kali.
DALILI
• Majani machanga hujikunja na baadaye majani yote.
• Kupungua kwa utoaji maua
na matunda na hata yakitokea matunda huwa ni madogo.
• Mmea kudumaa na kutozaa kabisa.
KUZUIA
Mbinu madhubuti ni kupunguza kuenea kwa ugonjwa huu kwenye
shamba kwa kudhibiti kuzaana na kuenea kwa mdudu (inzi mweupe) kama tulivyo ona katika kupambana na mdudu huyo, yaani:
• Kuondoa mimea michache iliyo shikwa na ugonjwa maana
wadudu hawa wanachukua ugonjwa huu kutoka mimea hii.
• Kutumia mbegu zilizo hakikishwa kuwa zinaweza kuvumilia
ugonjwa huu na kutoa mavuno mazuri.
• Usilime nyanya karibu na eneo lililo na mazao kama bamia,mipapai maana mimea hii huhifadhi inzi mweupe.
Kuua inzi weupe wanaofyonza nyanya na kusambaza virusi kwa kutumia madawa.
Tumia madawa kama vile Selecron, Decis, Karate
n.k.
• Epuka kuchanganya zao la nyanya na mazao mengine
yanayohifadhi hawa nzi kama vile mipapai na
bamia.
• Ng'oa na kuchoma moto mimea yote iliyougua ugonjwa huu.
UGONJWA WA KUOZA
SEHEMU YA SHINA INAYOGUSA UDONGO NA MMEMA KUNYAUKA KAMA UMEKOSA MAJI
• Wadudu wanaosabisha ugonjwa huu hupatikana ardhini.
• Hakuna dawa ya kutibu ugonjwa huu baada ya dalili
kujitokeza.
• Kupiga madawa za viwandani ardhini kabla ya kupanda nyanya
husaidia kupungu wadudu wa ugonjwa.
• Epuka kupanda nyanya au mazao jamii ya nyanya katika eneo
moja kwa muda mrefu mfulilizo. Baadhi ya mazao yanayohusiana na nyanya ni
bilinganya, pilipili, ngogwe, mnavu, n.k.
Ugonjwa wa miche michanga ya nyanya kuoza sehemu ya shina
inayogusa udongo na kufa ghafla
Ugonjwa huu hushambulia miche kitaluni na husabishwa na
wadudu waishio ardhini. Mara baada ya dalili, ugonjwa huu hauna dawa ila
unaweza kukingwa kwa kutumia njia zifuatazo:
• Choma moto udongo wa kutengenezea kitalu kabla ya kupanda
mbegu zako. Kutumia mboji husaidia kukinga miche dhidi ya ugonjwa huu.
• Epuka kumwagilia maji kupita kiasi na kutumia kuvuli
kizito
MATUNDA YA NYANYA
KUOZA KITAKO
Huu ni ugonjwa unaosababishwa na:
• Umwagiliaji wa nyanya bustanini usio na mpangilio maalumu.
Mfano, kumwagilia mimea maji mengi kisha kuiacha bila maji kwa siku kadhaa.
• Upungufu wa virutubisho aina ya chokaa. Dalili zake ni
matunda ya nyanya kuoza sehemu ya kitako na kuonyesha rangi nyeusi.
Kuzuia ugonjwa huu, zingatia kuwa na utaratibu mzuri wa
kumwagilia maji ambao haubadiliki ovyo kiratiba na kiasi cha maji
yanayowekwa. Rutubisha mimea kwa madini ya chokaa kwa
kutumia mbolea aina ya CAN zenye madini haya.
UPUNGUFU WA WADINI YA FOSFPRASI