Kuzingatia Ili Kuwa Na Maisha Yenye Furaha Na Mafanikio Makubwa

Karibu katika makala yetu ya leo tuweze kujifunza vitu ambavyo kila mtu anapaswa kuwa navyo ili kufikia mafanikio yake katika maisha ya kila siku. Ni vitu vya kawaida tu lakini vina nguvu kubwa sana kwa binadamu ni vitu ambavyo vinachochea mafanikio na kama unataka kufika katika kilele cha mafanikio katika safari yako hivi vitu ni kama nishati ya mafuta ambayo yanafanya gari lako liweze kutembea. Kama tunavyojua gari haliwezi kutembea bila ya kuwa na nishati vivyo hivyo kwa binadamu anahitaji kuwa na vitu hivi kama nishati yake katika safari ya mafanikio.

Pengine unaweza kujiuliza vitu hivyo nini? Vitu ambavyo kila mtu anatakiwa kuwa navyo katika maisha yake katika kufikia safari ya mafanikio ni kama ifuatavyo;

1. Upendo ; 
Maisha yako yakikosa upendo naweza kusema unaishi maisha ya ubinafsi, maisha ya chuki, upendo ukikosekana sehemu yoyote matokeo yake ni chuki na chuki huzaa mauti. Angalia jamii mbalimbali zinavyopata shida kwa sababu hakuna upendo zimetawala chuki tu. Upendo utaleta maendeleo katika jamii kama kila mtu akimfundisha mwenzake kile anachojua yeye ili naye aweze kufikia mafanikio.

Ukimpenda mwenzako kama unavyojipenda wewe tutapunguza umasikini wa kimawazo, kifedha nakadhalika kwa sababu mtu ambaye amefanikiwa akichukua jukumu la kuwasaidia wengine kimawazo ili nao wafikie kama yeye alivyofikia atakua amefanya upendo mkubwa sana hata Yesu Kristo alitoa amri ya mpya upendo kwa watu wote alivyokuja duniani. Hivyo basi upendo una nguvu kubwa katika maendeleo tuishi maisha ya falsafa ya upendo.

2. Amani ; 
Amani ni tunda ambalo tunatakiwa kulistawisha kila siku. Maisha bila amani ni sawa na kuhamisha maji katika bahari. Ziko jamii nyingi hapa duniani wanapata shida ya kutokufanya kazi kwa sababu jamii yao haina amani. Kama hakuna amani uchumi nao utashuka katika nchi, watu watashindwa kwenda kuzalisha na kufanya shughuli za kila siku matokeo yake hali inakuwa mbaya sana.

Waswahili wanasema nyumba usiyolala hujui ila yake hii ikiwa ina maana kwamba huwezi kujua umuhimu wa amani kwa sababu wewe unaishi katika nyumba ambayo haina amani. Kwa hiyo bila amani hakuna mafanikio ili binadamu aweze kuishi na kufikia mafanikio lazima amani iwepo kwanza. Faida za amani katika jamii yetu ni nyingi kuliko maelezo.

3. Furaha ;
Katika maisha ya mwanadamu furaha ndio inayomletea hamasa ya kufikia mafanikio. Waandishi wengi wa vitabu wanaandika furaha inaleta pesa na siyo pesa kuleta furaha. Ukiwa na furaha ya asili na na ya muda mrefu itakusaidia kukuletea mafanikio. Furaha itakuletea kufanya kazi kwa juhudi na maarifa kwa ufanisi mkubwa. Tusitafute furaha za muda mfupi bali tutafute furaha za muda mrefu. Furaha za muda mfupi ndio furaha ambazo zinawatesa watu kila siku mfano mtu amepatwa na tatizo anaona akienda kunywa pombe ndio atapata furaha ila baada ya kunywa na pombe kuisha anarudi katika hali ileile na matokeo yake unakuwa mtumwa wa kunywa vilevi vya kila aina ili uweze kupata furaha.

4. Imani; 
imani ina nguvu kubwa sana. Kila mtu anapaswa kuwa na imani na mambo anayofanya na kuwa na mafanikio katika mambo hayo anayoyafanya. Kama umekosa imani katika maisha yako basi umeanza kuwa na dalili ya kukata tama na kukata tamaa ni dhambi katika maisha. Unapaswa kuwa na imani chanya katika maisha yako hata kama umeanguka mara mbili amka na endelea na safari utayashinda maisha lakini ukiwa ni mtu wa kukata tamaa sahau mafanikio yoyote katika maisha yako. Ila kumbuka imani yako iendane na matendo yako kama una imani ya kushinda na kufanikwa basi jitihada za kufanya kazi zionekane na usitegemee kuvuna kama hujapata chochote.

5. Uvumilivu;
Mvumilivu hula mbivu ndio tusitegemee kupanda leo na kuvuna kesho kila jambo linahitaji uvumilivu kutokuwa na uvumilivu ni ngumu kwa mtu kufikia mafanikio yoyote. Watu wengi wanapenda kuona matokeo ya haraka sana katika kile wanachofanya mtu akiambiwa biashara Fulani inalipa basi anataka kuona mabadiliko ya haraka katika biashara yake hiyo. Kwa hiyo tunapaswa kuwa na uvumilivu ndio tunaweza kushinda katika maisha ya mafanikio. Ukiona mtu ana mafanikio ujue kabisa hajawekeza kwa siku moja alikuwa na uvumilivu ndio maana akafanikiwa. Tuishi maisha ya uvumilivu na tusitegemee mafanikio ya haraka mafanikio yanakwenda kama vile mtu anavyopanda ngazi anaanza chini kabisa mpaka anafikia pale alipokusudia kwenda .

6. Nidhamu; 
Nidhamu ni daraja katika mafanikio. Kama huna nidhamu katika maisha yako usitegemee kufanikiwa kwa sababu unaweza kuwa na vitu vyote lakini ukikosa nidhamu ni tatizo, huna nidhamu ya fedha halafu unataka mafanikio, huna nidhamu ya kujituma, kufanya kazi kwa bidii na maarifa halafu unataka mafanikio ni ngumu. Ukiwa na nidhamu utakua mwaminifu katika kazi zako kwa sababu nidhamu itakusukuma kufanya hivyo unatakiwa kuwahi eneo la tukio lazima uwe na nidhamu ya muda kufika eneo la tukio kwa uaminifu wa muda.

Hivyo basi, tunatakiwa tujiamini katika yale tunayofanya, kuwa na mtazamo chanya, tujifunze kwa bidii usiridhike na elimu yako uliyopata darasani tujifunze pia na elimu ambayo iko nje mtaala yaani non curriculum, tuache kulalamika ,tutumie muda vizuri na tukumbuke maisha ni muda.