Majimbo 10 yaliyotingisha uchaguzi Mkuu 2015

Hatimaye wababe wamepatikana katika majimbo 10 ya uchaguzi yaliyokuwa na ushindani mkali, hasa kati ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na CCM.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi tangu kuanza kwa kampeni Agosti 23, majimbo hayo yalikuwa na mvutano mkali ulioibua presha kubwa kwa vyama.

Wagombea katika majimbo hayo waliwekeza nguvu nyingi kuhakikisha wanayarejesha, wanayalinda au kuwaengua wenzao waliogombea tena katika majimbo husika.

Ilikuwa ni vita ya usiku na mchana kuhakikisha kuwa wanafanikiwa kuingia katika Bunge la 11 katika uchaguzi unaotajwa kuwa na ushindani mkubwa ambao ulifanyika Oktoba 25, Jumapili iliyopita huku baadhi ya majimbo, utangazaji wa matokeo ukichelewa kutokana na vuta nikuvute ya wagombea na wafuasi wa vyama.

Kilolo
Jimbo la Kilolo mkoani Iringa ni kati ya majimbo 10 yaliyokuwa na ushindani mkali. Jimbo hilo liliwaniwa na wagombea kutoka vyama vinne, Venance Mwamoto wa CCM, Taji Mtuga (ACT-Wazalendo), Brian Kikoti (Chadema) na Lameck Mgimwa wa Chausta.

Hata hivyo, upinzani mkali ulionekana kuwa kwa Mwamoto, ambaye alirejea tena kwenye kinyang’anyiro hicho baada ya kuenguliwa kwenye kura za maoni za CCM mwaka 2010, na Kikoti, ambaye nguvu yake ilitokana na kuungwa mkono na vyama vinne vinavyounda Ukawa vya Chadema, NCCR-Mageuzi, NLD na CUF.

Ushindani huo ulitajwa kuanzishwa na mpasuko ndani ya CCM ulitokana na kura za maoni. Baada ya Mwamoto kumshinda Profesa Peter Msolla, aliyekuwa mbunge, na baadhi ya makada wa chama hicho kutimikia Chadema.

Pamoja na mvutano huo Mwamoto aliibua mshindi kwa kupata kura 45,225 akifuatiwa na Kikoti aliyepata kura 32,926.

Iringa Mjini
Ni Jimbo jingine lililokuwa gumu kutabiri mshindi ambalo liliwaniwa na Robert Kisinini wa DP, Daudi Masasi (ADC), Mchungaji Peter Msigwa wa Chadema, Chiku Abwao (ACT Wazalendo) na Frederick Mwakalebelea wa CCM.

Kati ya wagombea wote ni Mchungaji Msigwa aliyetetea kiti chake na Mwakalebela ndiyo walioonekana kupambana vikali.

Mwakalebela alibebwa na falsafa inayotumiwa na CCM za kukomboa jimbo ambayo imefanikisha kuvunjwa makundi yaliyoundwa na wagombea wa nafasi hiyo wakati wa kura za maoni.

Katika kuonyesha umuhimu wa ushindi katika jimbo hilo mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa alikuwa wa kwanza kupita Iringa Mjini na kuvuta maelfu ya watu. Lakini Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli alifuta nyayo zake alipopita muda mfupi baadaye na kuzoa idadi kubwa ya wananchama na wapenzi.

Hata hivyo, Mchungaji Msigwa ndiye aliyeibuka mshindi katika uchaguzi huo baada ya kupata kura 43, 154 na kumbwaga Mwakalebela aliyepata kura 32,406

Kutokana na ushindi huo wa Chadema, msemaji wa kampeni CCM, January Makamba alisema chama hicho kitakata rufaa kwa maelezo kupinga matokeo hayo kwa kuwa kanuni za uchaguzi zilikiukwa.

Ilemela
Mkoani Mwanza, Jimbo la Ilemela lilikuwa na mchuano mkali kutokana na CCM kutaka kulirejesha kutoka Chadema waliolitwaa mwaka 2010. CCM ilimsimamisha Anjelina Mabula kupambana na mbunge aliyemaliza muda wake, Highness Kiwia wa Chadema.

Katika uchaguzi wa jimbo hilo uliokuwa na mvutano mkali huku wafuasi wa CCM na Chadema wakikesha kusubiri matokeo, Mabula aliibuka kidedea kwa kupata kura 85,424 dhidi ya kura 61,679 za Kiwia.

Bukoba Mjini
Ni kati ya majimbo ambayo wananchi walijitokeza kwa wingi katika mikutano ya kampeni ya Dk Magufuli na Lowassa.

Ushindani katika jimbo hilo ulikuwa mkali zaidi ya ule wa mwaka 2005. Jimbo hilo liliwakutanisha wagombea ambao ni mahasimu wakubwa, Wilfred Lwakatare wa Chadema, na Balozi Khamis Kagasheki wa CCM.

Wakati Kagasheki akitetea jimbo hilo kwa kipindi cha tatu, mshindani wake aliwatumia makada wa CCM waliohamia upinzani kujiimarisha kisiasa akiwamo aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dk Anatory Amani aliyehamia NCCR- Mageuzi iliyo ndani ya Ukawa.

Kundi la Dk Amani lililojiunga linaongezewa nguvu na aliyekuwa mwenyekiti wa UVCCM wa Manispaa ya Bukoba, Chifu Karumuna aliyehamia Chadema na kuongeza ushindani, huku Balozi Kagasheki akitajwa kuungwa mkono na wanawake wengi.

Hatimaye matokeo ya jimbo hilo yalitangazwa na Lwakatare kupata ushindi baada ya kupata kura 28, 112 na kumshinda Balozi Kagasheki aliyepata kura 25, 565.

Musoma Mjini
Mkoani Mara, vita kali ilionekana Jimbo la Musoma Mjini, kati ya Vincent Nyerere wa Chadema na Vedastus Mathayo wa CCM aliyeangushwa na mshindani wake huyo mwaka 2010. Jimbo hilo lilikuwa na wagombea tisa ambao ni Tongora Eliud (ACT-Wazalendo), Ibrahim Seleman (Tadea), Maimuna Matola (ADC), Ruttaga Sospeter (AFP), Mathayo (CCM), Nyerere (Chadema), Gabriel Ocharo (CUF), Nyakitita Chrisant (DP) na Makongoro Jumanne (UMD).

Mathayo alimuangusha mpinzani wake wa mwaka 2010 baada ya kupata kura 32, 836 huku Nyerere akipata 25, 549.

Moshi Mjini
Ushindani mwingine ulikuwa jimbo la Moshi Mjini, ambako wagombea wa CCM na Chadema walichuana vikali kumrithi Phillemon Ndesamburo ambaye ameamua kutogombea. CCM ilimsimamisha Davis Mosha na Jaffar Michael aligombea kupitia Chadema, kufanya uchaguzi wa mwaka huu kuwa na ushindani ambao haujawahi kuonekana tangu mwaka 1995.

Ushindani huo ulihitimishwa siku yalipotangazwa matokeo baada ya Jaffary kuibua kidedea kwa kupata kura 51,646 huku mpinzani wake Mosha akipata kura 26,920.

Kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayo ilizuka hali ya sintofahamu mjini Moshi na kuzua taharuki kwa wananchi.

Kawe
Jijini Dar es Salaam, nguvu ya Ukawa na CCM ilielelekwa Jimbo la Kawe ambako CCM ilimsimamisha Kippi Warioba wakati Chadema ikiendelea kumuamini mbunge aliyemaliza muda wake, Halima Mdee.

Ilielezwa kuwa Kippi alitegemea ushawishi wa baba yake, Jaji Joseph Warioba, ambaye mara kadhaa alisimama jukwaani kumpigia debe mwanaye.

Matokeo ya jimbo hilo yalitangazwa siku ya tatu baada ya wananchi kupiga kura kutokana na mvutano ulioibuka kati ya Kippi na Mdee. Wakati Kippi akishinikiza matokeo kuhesabiwa upya, Mdee aligoma kufunguliwa kwa masanduku ya kuhifadhia kura kwa maelezo kuwa matokeo yatachakachuliwa.

Hata hivyo, baada ya vuta nikuvute Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Kinondoni, Mussa Natty alimaliza sintofahamu hiyo na kumtangaza Mdee kuwa mshindi kutokana na kupata kura 96,432, huku Kippi akipata kura 83,061.

Ubungo
Jimbo la Ubungo pia lilikuwa na upinzani mkali kati ya mgombea wa Chadema, Saed Kubenea, ambaye ni mwandishi wa habari, na wa CCM, Dk Didas Masaburi, meya wa jiji aliyemaliza muda wake.

Kama ilivyokuwa na Kawe, utangazaji wa matokeo katika jimbo pia ulichelewa kutokana na sababu mbalimbali jambo lililosababisha baadhi ya wananchi kuandamana kushinikiza yatangazwe.

Akitangaza matokeo hayo, Natty, alisema Kubenea, amepata jumla ya kura 87,666 huku mpinzani wake Masaburi akipata kura 59,514.

Mbeya Mjini
Mbeya Mjini ni jimbo jingine lililokuwa na ushindani mkali kutokana na CCM kutafuta kila njia kulirejesha mikononi mwao, huku Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu wa Chadema akijichimbia zaidi baada ya kushinda mwaka 2010.

Katika kutafuta mtu wa kushindana na mgombea huyo kijana mwenye umri wa miaka 43, CCM ilimpitisha Samwee Shitambala ambaye mwaka 2005 aligombea kwa tiketi ya Chadema kabla ya kuenguliwa kwa kukosea kiapo.

Matokeo yalipotangazwa, Sugu aliibuka mshindi kwa kupata kura 97,775 dhidi ya 46,894 za Shitambala.

Bunda
Mpambano mwingine ulikuwa Jimbo la Bunda, ambako kulikuwa na vita ya vyama na umri. Mwanasiasa mkongwe, Steven Wasira (70) wa CCM alipambana na mbunge wa zamani wa viti maalumu (CCM), Ester Bulaya (35).

Bulaya aliamua kuondoka CCM kwenda upinzani muda mfupi baada ya Bunge kuvunjwa baada ya kulitumikia kwa kipindi kimoja akitokea Umoja wa Vijana wa CCM.

Upinzani kati ya Bulaya ya Wasira ulianza tangu wote wakiwa CCM, huku Bulaya akieleza wazi nia yake ya kujitosa katika kura ya maoni kuwania kupitishwa na CCM kugombea jimbo hilo, upinzani ambao uliendelea katika uchaguzi huo.

Bulaya alitangazwa mshindi kwa kura 28,508 akimbwaga Wasira aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, aliyepata kura 16,126.