UNYAMA! Zikiwa zimebaki siku 10 ili kupiga kura Oktoba 25,
mwaka huu katika uchaguzi mkuu, mgombea wa Udiwani Viti Maalum wilayani
Butiama, Mara kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) aliyetajwa
kwa jina moja la Upendo (39), anadai kutekwa na kundi la vijana wapatao 105
kisha kubakwa na kuachwa katika hali mbaya
ILIKUWA SAA 11:30
JIONI
Tukio hilo la kinyama na kikatili lilijiri Oktoba 7, mwaka
huu, saa 11:30 jioni katika Kijiji cha Butuguri wilayani Butiama ambapo mgombea
huyo alikumbwa na mkasa huo baada ya gari la mgombea ubunge wa Jimbo la Butiama
kupitia Chadema, Yusufu Khazi alilokuwa akisafiria kushambuliwa na kuvunjwa
vioo na taa.
Kwa mujibu wa mashuhuda, gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser lenye
nambari za usajili T 973 AEV lililokuwa likiendeshwa na Masembo Paulo
liliwabeba baadhi ya viongozi na wanachama wa Chadema wakitokea kwenye mkutano
wa kampeni za ubunge katika Kijiji cha Sirorisimba ambapo mgombea wao wa ubunge
yeye aliondoka na helikopta ‘chopa’
UVAMIZI
Ilidaiwa kwamba, gari hilo
lilipofika Butuguri ndipo likavamiwa na vijana hao ambao walirusha mawe na
kuvunja vioo, taa na kuwajeruhi watu tisa waliokuwa ndani ya gari hilo kabla ya kumfanyia
unyama mgombea huyo.
AOKOTWA HOI
Ilielezwa kwamba, baada ya kumfanyia unyama huo, jamaa hao
walimuacha akiwa hoi ndipo akaokotwa na wasamaria wema ambao walimkimbiza
katika Hospitali ya Wilaya ya Butiama kwa ajili ya matibabu.
Akifafanua zaidi juu ya tukio hilo ,
Florah Tumaini Ryana, mgombea ubunge wa Viti Maalum katika jimbo hilo kupitia Chadema ambaye alikuwa ndani ya gari hilo na kunusurika baada ya kutoroka kwa kukimbia,
alieleza kwamba, anahisi vijana hao waliandaliwa mahususi kwa ajili ya tukio hilo .
WALIOJERUHIWA
WAFUNGULIWA MASHTAKA
Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida, inadaiwa kuwa
majeruhi tisa walijikuta wakifunguliwa mashtaka na viongozi wa chama kimoja cha
upinzani kuhusiana na tukio hilo hali iliyozua
maswali miongoni mwa wakazi wa eneo hilo .
Kesi hiyo yenye namba BUT/IR/830/2015 –SHAMBULIO
ilifunguliwa kwenye Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Butiama.
Katika jalada la kesi hiyo, watu hao tisa wanatuhumiwa
kuvamia kambi hiyo wakiwa na mapanga kwa lengo la kuwawekea vijana hao sumu
kwenye chakula.
POLISI WATHIBITISHA
Habari kutoka ndani ya kituo hicho cha polisi zilieleza
kwamba, waliojeruhiwa na kufunguliwa mashtaka kituoni hapo ni John Simba Mzuzu
(Katibu Mwenezi wa Chadema Wilaya ya Butiama), Pendo Juma (Diwani Viti Maalum
Kata ya Sirorisimba) na Yasinta Hassan (Diwani Viti Maalum Kata ya Kukirango).
Wengine ni Semi Jumanne (Mwanachama wa Chadema), Edson Kanza
(Mwanachama wa Chadema), Sospeter Mruta (Katibu Baraza la Vijana wa Chadema
Wilaya ya Butiama), Masemba Paulo na Siliakusi Rashid.
Kwa upande wao polisi wilayani Butiama walithibitisha
kutokea kwa tukio hilo
lililoripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Butiama na kwamba wanaendelea na
uchunguzi zaidi.
ASIMULIA MKASA MZIMA
Kwa upande wake mgombea huyo, akiwa na maumivu makali katika
kituo hicho cha polisi, alilisimulia Amani mkasa mzima kwamba, alishangaa
walipofika kijijini hapo kuona kundi la vijana hao waliokuwa na silaha za jadi
waliwavamia kisha kuwateka na kuanza kuwashushia kipigo.
“Walikuwa vijana kama 105
hivi, walituvamia kisha wakatuteka lakini wenzangu walifanikiwa kukimbia.
“Walinishika na kuanza kunibaka na walipoona nimezimia ndipo
wakakimbia.
“Ukweli wameniachia majeraha na maumivu makali
yasiyosimulika. Nawaomba watu wa haki za binadamu wanisaidie ili sheria itende
hali yake kwa sababu huu ni unyanyasaji wa kijinsia,” alisimulia Pendo nje ya
kituo cha polisi huku akitokwa machozi.
MKUU WA WILAYA ANENA
Akizungumzia tukio hilo , Mkuu
wa Wilaya ya Butiama ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya
Wilaya, Annarose Nyamubhi alikiri kutokea kwa tukio hilo .
“Hilo
tukio lipo lakini siwezi kulizungumzia zaidi kwa sababu lipo mikononi mwa
polisi,” alisema Annarose.
KAMANDA WA POLISI
Gazeti hili lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya
Rorya, ACP Philip Kalangi ili kuthibitisha tukio hilo alisema yupo nje ya mkoa ila
atalifuatilia.
