Kampeni za ubunge Jimbo la Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro,
zimeingia katika hatua nyingine baada ya wagombea kuanza kujinadi nyumba kwa
nyumba, mtu kwa mtu, mtaa kwa mtaa kwa lengo la kuhakikisha wanashinda Oktoba
25.
Mgombea wa CCM, Davis Mosha, amekuwa akitembea kwa miguu
mitaani kuomba kura huku wa Chadema, Jaffar Michael, akipita nyumba kwa nyumba.
Mgombea ubunge wa ACT-Wazalendo ambaye bado hajazindua
kampeni zake rasmi, Buni Ramole, amejikita zaidi kwenye kampeni za chini kwa
chini.
Mosha aliliambia gazeti hili kuwa kampeni ya mtu kwa mtu
anayoifanya ina ushawishi mkubwa ikilinganishwa na mikutano ya majukwaani kwa
vile inamfikia hata asiyehudhuria mikutano.
“Safari hii tumewashika pabaya na tutaendelea na kasi hii,
tutashambulia majukwaani na tutashambulia mitaani na tutashambulia nyumba hadi
nyumba na mtu hadi mtu, hakuna kulala,” alisema Mosha.
Mmoja wa makampeni meneja wa Michael, Peter Kimaro, alidai
CCM wameiga mbinu zao kwani wao ndiyo walianza kuzunguka kata moja hadi
nyingine.
“Wao wametuiga sisi tumekuwa tukimpangia mgombea wetu
kuzunguka kata moja hadi nyingine na kujipenyeza kwenye mikusanyiko ya watu.
Tulianzia Bondeni, Soko la Mbuyuni na Korongoni,” alidai Kimaro.
Alisema mbali na kumtembeza mgombea wao nyumba hadi nyumba,
lakini bado wataendelea kutumia magari ya matangazo kuzunguka kwenye maeneo ya
pembezoni kumnadi kwa wananchi.
Ramole alisema atazindua rasmu kampeni zake za ubunge baada
ya kuzinduliwa za madiwani.
“Hata zikibaki siku kumi nitazindua tu, ila kampeni
ninayoifanya sasa ni zaidi ya uzinduzi rasmi wa jukwaani,” alisema Ramole.
