Mahakama ya Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani imemhukumu Shaban Rashid Mlanga, Miaka 22, Mkazi wa Zinga Wilayani Bagamoyo kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Hukumu hiyo imetolewa Agosti 5 2026 mbele ya hakimu wa mahakama hiyo Mhe. Felister Ngw’elu baada ya kujiridhisha na ushahidi uliotolewa pasipo na shaka kuwezesha kumtia hatiani mshtakiwa huyo.
Akisoma hukumu hiyo Mhe. Felister alisema mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo Februari 12, 2026 majira ya saa 10:00 jioni huko maeneo ya Mwanalugali Wilaya ya Kibaha ambapo alimchoma mwanamke mmoja kisu nyuma ya mgongo na kumuibia simu aina ya Infinix Hot 12 yenye thamani ya shilingi 250,000.
Mara baada ya kesi hiyo kuripotiwa kituo cha Polisi Kibaha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani lilifanya jitihada za kumkamata mtuhumiwa na upelelezi kuanza mara moja kisha kufikishwa makahakami.
Mhe. Felister ametoa adhabu ya Kifungo cha jela miaka 30 kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha chini ya kifungu namba 287 A kanuni ya adhabu Sura ya 16 kilichofanyiwa marejeo mwaka 2023.
