Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Kenya, IEBC, imechapisha kanuni mpya za ufadhili wa kampeni pamoja na viwango vya juu vya matumizi ya fedha, huku wagombea na vyama vya kisiasa wakianza maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Katika notisi iliyochapishwa katika Gazeti rasmi la serikali ya Kenya ya tarehe 7 Agosti 2026, IEBC imeweka kikomo cha matumizi ya kampeni za mgombea urais kuwa Sh 6.11 bilioni.
Kwa mujibu wa tume hiyo, viwango hivyo vimeamuliwa kwa kutumia kanuni inayozingatia idadi ya watu na ukubwa wa eneo, ambapo idadi ya watu ina uzito wa asilimia 70 na eneo la ardhi asilimia 30.
Viwango hivyo vinahusu uchaguzi wa urais, magavana, wabunge wa Bunge la Kitaifa na Wawakilishi wa Kaunti, pamoja na vyama vya kisiasa vitakavyoshiriki katika uchaguzi huo.
IEBC pia imeweka kikomo cha jumla cha matumizi ya vyama vya kisiasa kuwa $189.6 milioni.
Chini ya kanuni hizo mpya, mtu mmoja au chanzo kimoja hakitaruhusiwa kutoa zaidi ya asilimia 20 ya jumla ya michango inayoruhusiwa kwa mgombea au chama husika.
Tume imeonya kuwa wagombea au kamati za vyama vya kisiasa zitakazozidisha viwango vilivyowekwa na kushindwa kuripoti ukiukaji huo zitakuwa zimefanya kosa la jinai.
''Mtu atakayepatikana na hatia anaweza kutozwa faini ya hadi Sh2 milioni, kifungo cha hadi miaka mitano jela, au adhabu zote mbili'', yasema IEBC.
IEBC imewataka vyama vya kisiasa, wagombea, timu za kampeni, wafadhili na watu wengine wanaodhibitiwa na sheria hizo kuanza kufahamu mara moja masharti kuhusu michango na matumizi ya kampeni, utunzaji wa kumbukumbu, utoaji wa taarifa na uwajibikaji.
