Watu sita wafa ajalini Mikumi mkoani Morogoro

Watu sita wamepoteza maisha baada ya gari waliyokuwa wanasafiria kugongana uso kwa uso na basi linalomilikiwa na kampuni ya Prince Muro.

Ajali hiyo imetokea leo eneo la Mikumi majira ya saa sita kasorobo baada ya gari aina ya Noah  lililokuwa linatoka mikumi kwenda Morogoro Mjini kupasuka tairi la mbele (kulia), kupoteza mwelekeo na kisha kugongana na basi la Prince Muro lililokuwa linatoka Dar es Salaam kuelekea Tunduma mkoani Mbeya.

Kamanda wa Polisi mkoani Morogoro, Leonard Paul amewaambia waandishi wa habari mjini humo kuwa katika ajali hiyo watu wote sita waliokuwa wanasafiri kwa Noah hiyo walifariki dunia papo hapo huku baadhi ya abiria wa basi la Prince Muro wakipata majeraha madogo.

Kamanda Paul amesema kati ya marehemu sita wa ajali hiyo, wanne ni wanaume na wawili ni wanawake.

Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya mkoa wa Morogoro ikisubiri utambuzi na kwamba majeruhi wametibiwa katika hospitali ya Mtakatifu Kizito iliyopo mjini Mikumi na kuruhusiwa kuendelea na safari.

Amesema baada ya ajali kutokea jeshi lake lilifanya upekuzi kwenye Noah na kufanikiwa kupata vitambulisho vinne na kusema vitasaidia katika mchakato wa kuwatambua marehemu.

Akizungumzia chanzo cha ajali hiyo, Kamanda Paul amesema mashuhuda wa ajali hiyo wamesema dereva wa Noah alikuwa kwenye mwendo kasi hivyo kushindwa kulimudu gari mara baada ya tairi kupasuka.