Bond amwangukia Wastara

 Aliyekuwa mchumba wa mwigizaji wa staa wa sinema za Kibongo, Wastara Juma, Bond Suleiman.

Msamaha! Aliyekuwa mchumba wa mwigizaji wa staa wa sinema za Kibongo, Wastara Juma, Bond Suleiman amemwangukia mwandani wake huyo na kumuomba amsamehe kwani vitendo alivyokuwa akimfanyia vilitokana na kurogwa na wanawake aliowahi kutoka nao kimapenzi akiwemo msanii wa filamu, Lulu Semagongo ‘Aunty Lulu’.

Akizungumza na Ijumaa Wikienda kwa njia ya simu akiwa Saadan wilayani Bagamoyo, Bond alifunguka kuwa anamuomba Wastara amsamehe kwani amemkosea mengi na hayo yote hayakuwa ni makusudi yake bali kurogwa na Aunty Lulu pamoja na mwanamke mwingine aliyemtaja kwa jina moja la Saida.

Bond alidadavua kwamba, kwa siku hamsini alizokaa kwenye maombi huko Saadan amebadilika na kuachana na maisha ya ufuska aliyokuwa akiishi zamani hivyo anaomba msamaha kwa Wastara na kwa sababu amemtesa, anajutia makosa yake.

“Namuomba Wastara usiku na mchana anisamehe na nikitoka huku nitapita kwenye vyombo vya habari ili dunia nzima isikie na sitarudia tena, nimekuwa mwema na mpole, nimeamua kurudi kwa Mungu wangu, nampongeza Wastara kwa kunivumilia.

“Namuomba anihurumie kwani nilikuwa natumiwa na shetani kufanya mambo machafu,” alisema Bond.

Baada ya kusikia maombi ya Bond, Ijumaa Wikienda liliyafikisha kwa Wastara ambapo alifunguka:
“Bond aiambie dunia nzima na awaahidi mashabiki wangu na aseme hukumu yake kabisa siku akinigeuka, anipe muda halafu sitaki aniguse, aongoze kwetu na familia yake kama anataka mke siku nikiwa tayari na ni baada ya kuhakikisha afya zetu ziko salama.”

Kwa upande wake Aunty Lulu alipoulizwa kuhusiana na tuhuma za kumroga Bond alifunguka: “Nimroge Bond kwa lipi? Nishindwe kuroga maisha yangu nikahangaike na mtu?”