DALILI ZA SARATANI YA KOO

DALILI ZA SARATANI YA KOO
1.Siku za mwanzo mgonjwa anaweza kushindwa kumeza chakula kigumu kisha cha majimaji na baadaye akashindwa kumeza hata mate
2.Maumivu wakati wa kumeza chakula hasa chakula kigumu
3.Maumivu kwenye kifua au mgongoni
4.Kupungua uzito
5.Kiungulia
6.Sauti ya mkwaruzo au kikohozi kikavu cha zaidi ya wiki mbili

Hata hivyo ifahamike kuwa dalili hizi zinaweza kutokea pia kwa baadhi ya magonjwa mengine tofauti na saratani ya koo. Hivyo ni vizuri kumuona daktari kwa uchunguzi zaidi.

UCHUNGUZI NA VIPIMO
Vipimo kwa ajili ya utambuzi wa saratani ya koo ni pamoja na
Aina ya X ray iitwayo Barium swallow ambayo huonesha muundo wa koo pamoja na tumbo (stomach).

Kipimo cha Endoscopy ambacho husaidia kuchunguza ndani ya koo, tumbo pamoja na eneo lote la utumbo Kuchunguza sehemu ya koo kwenye darubini (biopsy). Kwa sasa, njia hii ndiyo ya uhakika zaidi ya kutambua uwepo wa seli za saratani katika koo.

Iwapo itathibitika kuwepo kwa saratani katika koo, madaktari hupendelea kufahamu hatua ya ugonjwa ilipofikia. Kitendo hiki huitwa staging. Faida ya kufanya staging ni kuwa husaidia kufahamu ukubwa wa tatizo yaani ni kwa kiasi gani seli za koo zimeathiriwa, iwapo saratani imesambaa na kuathiri maeneo ya jirani na kama imesambaa ni viungo gani vilivyo athirika.

Aidha staging husaidia pia kufanya maamuzi ya njia gani ya tiba itumike katika kumtibu mgonjwa. Saratani ya koo huweza kusambaa na kuathiri sehemu kama mifupa, ini na mapafu.

Ili kufahamu kama saratani imesambaa kwenye viungo hivi, vipimo vifuatavyo vyaweza kufanyika:
Kipimo kiitwacho endoscopic ultrasound ambacho husaidia kutambua iwapo viungo vilivyo jirani na koo vimeathirika ama la. Pia husaidia kufahamu hali ya tezi (lymph nodes) zilizo karibu na koo. Daktari pia anaweza kuchukua sehemu ya tezi hizo (lymph node biopsy) kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

CT Scan husaidia kutambua jinsi koo na sehemu nyingi za mwili zilivyoathirika.
MRI ni kipimo kingine kinachosaidia kuonesha iwapo saratani ya koo imesambaa na kuathiri tezi na sehemu nyingine za mwili.

PET scan: Nia aina ya kipimo ambacho huonesha kwa uhakika na ubora zaidi ukilinganisha na vipimo vingine uwepo wa saratani ya koo na kama imesambaa sehemu nyingine za mwili. Hata hivyo, kipimo hiki kwa sasa hakipatikani nchini kwetu.

Bone scan ni kipimo ambacho huwezesha kutambua iwapo saratani imesambaa mpka kwenye mifupa.TUTAENDELEA PANAPO MAJALIWA.