NJIA KUU TANO ZA KUONGEZA UZALISHAJI WAKO

Linapokuja swala la muda wa uzalishaji(productive time), kuna tofauti kubwa baina ya watu. Kila mtu ana muda wake ambao anakuwa na uwezo wa kufikiri vizuri na kufanya mambo makubwa na kwa ubunifu mkubwa. Kuna ambao muda wao mzuri ni usiku sana na kuna ambao muda wao mzuri ni asubuhi na mapema na wengine katikati ya siku.

Je wewe unajua muda ambao unakuwa na uzalishaji wa hali ya juu? Ni muhimu sana kuujua muda wako maana kutokujua ni chanzo cha kupoteza muda wako mzuri wa kuzalisha.

Siwezi kukueleza hapa muda wako ni mzuri wakati gani bali hii inaweza kufanyika na wewe mwenyewe. Kama hujawahi kujitathmini na kujua muda wako mzuri chukua siku kadhaa na jaribu kufanya kazi inayokuhutaji kufikiri na kutoa ubunifu kwa nyakati tofauti za siku. Jaribu kufanya hivyo usiku sana, asubuhi sana na nyakati nyingine za siku. Ule muda ambao unaona unakuwa tayari kufanya kazi vizuri na mawazo yanatiririka bila kikomo ndio utakaokuwa muda wako mzuri.

Baada ya kujua muda ambao unakuwa na uzalishaji wa hali ya juu ni vyema ukajua jinsi ya kuutumia muda wako vizuri ili kupata uzalishaji mzuri. Kuna mambo muhimu matano ya kufanya kwenye muda wako mzuri wa uzalishaji.

1. Kuwa na mipango kabla ya muda haujafika. Kama muda wako mzuri ni asubuhi na mapema basi ni vyema kabla hujalala ukajua ukiamka unafanya nini. Kama usipokuwa na mipango, muda unapofika unaweza kujikuta unapoteza muda mwingi kufikiria unafanya nini na unafanya kwa njia gani.(soma; kabla hujalala fanya hivi)

2. Fanya jambo moja kwa wakati mmoja. Kuna wakati huwa tunafikiri kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja ni kuokoa muda ila kiuhalisia ni kupoteza muda. Unapofanya mambo mengi kwa wakati mmoja unapunguza ubunifu na ufanisi. Fanya jambo moja ukitumia akili yako yote, likiisha anza jingine. Kwa njia hii utajikuta unamaliza mambo mengi ndani ya muda mfupi.

3. Ondoa mazingira yoyote ya kukuvuruga. Hapa ndio pagumu kuliko sehemu zote. Mara nyingi huwa tunafikiri kufanya kazi huku ukisikiliza muziki ama kuangalia tv, ama kuwa kwenye mitandao ya kijamii ni njia ya kutuchangamsha. Ukweli ni kwamba kama kuna chochote kinachohamisha mawazo yako kutoka kwenye jambo unalofanya kinapunguza ufanisi wako. Ukisoma huku unasikiliza muziki kwa masaa manne, unakuwa umezediwa na aliesoma akiwa sehemu tulivu kwa masaa mawili. Hivyo unapokuwa kwenye muda wako wa uzalishaji zima kelele zozote na ondoa kabisa internet kwenye computer yako(kama unatumia kompyuta)

4. Jifunze kusema hapana. Unaweza kuwa uko kwenye muda wako mzuri na unafanya kazi zako kisha anatokea rafiki yako anakwambia labda muende mkale, au mkatembee au mkafanye chochote ambacho kinamfurahisha huyo rafiki yako kwa wakati huo.

Unaweza kuwa unampenda sana, ila kwa faida yako na yake mwambie hapana na jaribu kumpa sababu za msingi zinazokufanya usiweze kutoka muda huo. Kwa njia hiyo atauelewa utaratibu wako na siku nyingine hatokusumbua tena, ila ukifanya unafiki wa kwenda tu ili kumfurahisha unapoteza muda wako na mara nyingi ataendelea kukukwamisha.

5. Potea. Kama inakuwia vigumu kuwakatalia watu wakati wa muda wako wa uzalishaji, njia nzuri ni kupotea kabisa kwenye huo muda. Unaweza kuwa na sehemu ambayo hakuna atakaejua ulipo, kuzima simu na hutokuwa kwenye mtandao kabisa(kama kipindi cha chimbo mashuleni). Ukiweza kupata masaa mawili ya kufanya mambo yako itakuwa vizuri sana kwako na hakuna unachoweza poteza kwa muda huo mfupi utakaopotea.

Shughuli yoyote ambayo inahitaji kufikiria na ubunifu wa hali ya juu ni vyema ukaifanya kwenye muda ambao uzalishaji wako ni wa hali ya juu. Na pia ni vyema ukautumia muda huo vizuri ili kuweza kunufaika na kuyafikia malengo yako.