Serikali yafunga mpaka usio rasmi katika eneo la Gosebe mkoani Mara

Serikali wilayani Tarime mkoani Mara imeufunga mpaka usio rasmi katika eneo la Gosebe walayani humo ambao unadaiwa kuingiza bidhaakwa njia za panya kati ya nchi za Tanzania na Kenya bila kulipia ushuru na kodi mbalimbali.

Mpaka huo wa Gosebe ambao upo jirani kabisa na mpaka rasmi wa Sirari umekuwa ukitumika kuingiza bidhaa yakiwemo Mahindi nchini sanjari na kutumiwa na wafanyabiashara kutorosha bidhaa mbalimbali kwenda nje ya nchi kinyume cha sheria za nchi.

Mkuu wa wilaya ya Tarime Bw Glorious Luoga, akizungumza baada ya kutembelea eneo hilo na kushuhudia tani za mahindi yakiingizwa nchini, amesema mbali na mpaka huo kutumika kuingiza na kutoroshea bidhaa kwenda nje ya nchi lakini pia unaweza kuwa na madhara makubwa kiusalama.

Naye mmoja ya madiniwani wa nchi ya Kenya Bw Joseph  Hoyo, akizungumza na viongozi wa wilaya ya Tarime, amesema kuwa waliamua kutumia mpaka huo kwa ajili ya kuingizia mahindi Tanzania ili yauzwe kwa baadhi ya maeneo yenye upungufu wa chakula nchini,  huku baadhi ya vijana wakidai kufungwa kwa mpaka huo kutawakosesha ajira katika eneo hilo.