Kigera wamuomba Lukuvi kunusuru nyumba za maskini

Wakazi wa Kata ya Kigera, Manispaa ya Musoma mkoani Mara wamemuomba Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kusaidia kutatua mgogoro wa ardhi.

Wamedai mgogoro huo unatokana na ujenzi wa barabara unaoendelea kwenye kata hiyo kuegemea upande mmoja ambao una nyumba za watu wa hali ya chini na kuacha zile za matajiri.

Baadhi ya wakazi hao waliwaambia waandishi wa habari kuwa, wameishi katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka 30 na kwamba, barabara iliyokuwa ikitumika inajulikana lakini ujenzi unaoendelea umefika katika makazi yao.

Walisema waliwasilisha malalamiko yao kwa viongozi wa mipango miji waliokuwa wakipima barabara hiyo, lakini hawakuwasikiliza isipokuwa waliendelea kuweka mchoro ambao unaegemea upande mmoja.

“Barabara hii ilikuwapo, tulikuwa tukiitumia siku zote. Cha kushangaza ni kwamba wanataka kuanza kukarabati, lakini wanakuja upande ambao una nyumba za watu wa hali ya chini na upande wenye nyumba za matajiri kuachwa bila kuguswa,” alisema Kelia Mkika.

Aisha Ramadhan alisema barabara hiyo inatakiwa kutengenezwa kwa kuegemea pande zote mbili na pia walitakiwa walipwe fidia kwa madai kuwa imewafuata.

Alisema Serikali inapaswa kuwasikiliza na kufanyia kazi malalimiko yao na kuwa, kutowasikiliza ni sawa na kuwapuuza.

“Tunaona hatusikilizwi, lakini tuna madai muhimu na yanayoeleweka. Labda wakubwa wameamua kutupuuza kwa sababu ya hali duni tulizo nazo,” alisema Ramadhan.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Khalfan Haule alithibitisha kuwahi kusikia malalamiko ya wakazi hao na kufafanua kuwa mchoro wa barabara hiyo unafuata vigingi vilivyowekwa mwaka 1990 na hakuna upendeleo kama wanavyodai.