Kushuka kwa Kiwango cha Elimu

Waziri wa Elimu,Sayansi,Teknolojia na Ufundi Professa Joyce Ndalichako amesema kasi ndogo ya uwajibikaji na utendaji kazi kwa taasisi na mamlaka za Elimu Nchini vimechangia kwa kiasi kikubwa kuzorota na kushuka kwa kiwango cha elimu hapa nchini na hivyo kusababisha wanafunzi wengi kutojua kusoma na kuandika katika Shule nyingi.

Profesa Ndalichako ameyasema hayo alipotembelea Taasisi ya Elimu Tanzania TET na kupata nafasi ya kuzungumza na menejimenti ya taasisi hiyo ambapo ameitaka kuongeza kasi ya utoaji elimu bora yenye viwango mashuleni pamoja na kuwapa mwongozo imara walimu utakaowawezesha kufundisha katika viwango vinavyotakiwa.

Amesema kuwa inashangaza kuona wanafunzi wengi wa shule za awali pamoja na za msingi hawajui kusoma na kuandika hali inayosababisha wengi wao kushindwa kuendelea na masomo ya juu na kulikosesha taifa wataalam na wasomi.

Aidha ameitaka Taasisi hiyo kuweka utaratibu wa haraka wa uchapishaji vitabu vya kutumia mashuleni ili viweze kusambazwa kwa wakati.

Wakati huohuo Waziri wa Elimu Sayansi Teknolojia na Ufundi Prof Joyce Ndalichako amezuru Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi NACTE ambapo amelitaka kutoa usajili wa vyuo kwa kuzingatia viwango kwa lengo la kuhakikisha vyuo hivyo vinatoa elimu bora itakayosaidia kuongezeka kwa vijana wengi wenye ujuzi nchini.