Machozi ya Aisha wa Zanzibar kwa watoto wake kubakwa

Vitendo vya ukatili wa kijinsia vimeendelea kuwa mwiba kwa watoto visiwani Zanzibar, huku wengi wakiendelea kuugulia maumivu ya ndani kwa ndani pasipo kuainisha matatizo yao kwa uwazi ndani ya jamii wanazoishi.

Mikoa ya Kusini na Kaskazini Unguja likiwamo eneo la Pwani Mchangani ni baadhi ya maeneo ambayo sehemu ya wakazi wake hasa wanawake na watoto wamekumbana na vitendo vya kikatili na unyanyasaji wa kijinsia.

Licha ya kukumbana na vitendo hivyo vinavyojumuisha kubakwa kwa wanawake na watoto wenye umri kati ya miaka miwili na nusu hadi 12 kulawitiwa, watuhumiwa wa makosa hayo wamekuwa wakiachiwa huru baada ya mashitaka waliyofunguliwa vituo vya polisi kufutwa bila kufikishwa mahakamani.

Kati ya wanawake waliokumbwa na unyama huo, Mama Aisha (si jina lake halisi) amekumbwa na kizaa zaa hiki baada ya watoto wake wawili kulawitiwa na baba yao mdogo zaidi ya mara tatu kila mmoja kwa nyakati tofauti.

Baada ya mwandishi wa makala haya kufika Pwani Mchangani, alibaini kuwapo hali isiyo ya kawaida kwa watoto hao na baada ya mazungumzo nao, kwa nyakati tofauti walimsimulia jinsi baba yao mdogo alivyokuwa akiwatendea kisha kuwatishia iwapo wangesema lolote.

Mama wa watoto hao akisimulia kisa kilichoisibu familia yake, anasema mwaka 2014 akiwa safarini, nyumbani kwake ilizuka tabia isiyopendeza ambayo ndugu wa familia ya mumewe iliwatendea watoto wake wawili wa kike.

Aisha anasema alivyosafiri alimuomba mumewe awapeleke watoto kwa baba yake, lakini alimkatalia na kwamba wiki mbili baadaye alimpigia simu na kumsihi arudi, akidai watoto wanapata tabu.

“Nilipofika Zanzibar watoto walinipokea vizuri, niliingia chumbani kwangu kupanga vitu, mwanangu mdogo akanifuata na kuanza kuniambia ‘basi mama ulipokuwa haupo basi Babu Ali ananivua chupi ananitia cheche, anayo kwenye suruali yake ananiweka huku’ nilimpima mpaka mtoto aliponijuza kwa uhakika,” anasema Mama Aisha aliyekuwa akiishi nyumba ya familia ya mumewe.

Anasema alipomhoji zaidi mtoto alipofanyiwa kitendo hicho alijibiwa ni chumbani kwa bibi yake na wakati mwingine vichakani, hali iliyomshitua akaanza kuhoji zaidi bila kuwa na wazo kama mdogo naye alifanyiwa kitendo hicho.

Akisimulia, Aisha anasema siku aliyorejea nyumbani watoto wake waliogeshwa kwa bibi yao, lakini siku ya pili kila alipokuwa akiwaogesha walikuwa wakilia, huku wakitokwa na uchafu sehemu za siri.

Anasema siku ya tatu mtoto wake mdogo akapata homa kali na kumpeleka hospitali kwa matibahu licha ya baba yake kutoafiki.

“Nilipofika hospitali wakapimwa, daktari akasema ana homa, akagundua kwamba mtoto ameingiliwa, akathibitisha kwamba ni kweli,” anasema.

Aisha anasema yeye na nduguze walikwenda Kituo cha Polisi Mkokotoni kufungua kesi, baada ya kurudi wakwe zake walimuita na kumuambia hayo ni mambo ya kifamilia yaachwe. Baadaye kesi ikafutwa.

Mara ya pili
“Siku moja nilikwenda shamba, niliporudi nilimuogesha mwanangu mdogo nikagundua ameingiliwa tena, nilipoenda kushitaki kwa wakwe, shemeji yangu alihamaki aliposikia nimeripoti kwa mara nyingine baada ya mara ya kwanza kuniambia niache ni masuala ya kifamilia,” Aisha anasimulia huku akitokwa na machozi.

Anasema aliamua kwenda kushtaki Kituo cha Polisi Mkokotoni, kisha shemeji yake kukamatwa na kutiwa mbaroni kwa siku mbili na kutolewa.

Anasema kesi hiyo ilipelekwa mahakamani, lakini shemeji yake huyo alihukumiwa kwa kutozwa faini ya Sh400,000 ambayo hata hivyo hakuambuliwa hata senti moja, huku mumewe akimuambia aende Mahakama ya Mfenesini kwa kupita mlango wa nyuma.

“Aliniambia nikifika niseme mimi ndiye niliyeitwa, nikamuambia sina taarifa yoyote kutoka kwa Sheha hivyo siwezi kwenda. Hebu hukumu faini 400,000, wanangu kuingiliwa ni sawa na hukumu hii?” Aisha anasema kwa uchungu huku akibubujikwa machozi.

Awamu ya tatu
Aisha anasema baadaye watoto wakawa hawataki kwenda kwa bibi yao, lakini siku moja aliondoka nyumbani, aliporejea mmoja wa watoto hao alimkimbilia na kumueleza kuwa aliingiliwa tena na baba yake mdogo.

“Nilianza kupiga yowe, nilipata uchungu mkubwa, nilimuangalia mwanangu na kumkataza asiende chooni wala kutawaza, sikumuogesha ili nimpeleke polisi kesho yake akiwa na kidhibiti. Usiku ukaingia akalala vilevile.”

“Kesho yake wakwe wakaniambia nimswalie Mtume, nisiende popote. Mume akasema nisubiri, nikasema naenda kwenye vyombo vya sheria, wakazuia milango nisitoke mpaka usiku ukaingia. Nilishinda njaa kwa siku mbili, nikiwa na wanangu.”

“Nilimshauri mume wangu tuondoke akakataa, mchana wake nikiwa chumbani na watoto, shemeji akaja. Akaingia, akawasukuma watoto, akaja kunipiga na kunivua nguo zote. Aliniacha uchi, wifi yangu akaja kunipa dera nivae, shemeji akatoka nje na kuanza kutukana, majirani wakajaa. Akaenda shambani kwangu na kung’oa mahindi yote, kunde hata njugu nilizopanda,” Anasimulia Aisha huku machozi yakitiririka mashavuni mwake.

Anasema siku ya tatu alipoona mumewe hajali chochote, alibeba watoto wake na kuondoka mpaka kwao kwa nauli alizoomba barabarani.

Anasema: “Nikafungua kesi, ikapelekwa Mahakama ya Mfenesini, tangu mwaka huu mwanzoni hadi sasa, nimekata tamaa maana sijui nini kinaendelea, sina fedha za nauli kufuatilia kesi hii.”

Upande wa familia ya mumewe ulipotafutwa kuzungumzia tuhuma hizo, alipatikana kaka wa mume wa Aisha ambaye anasema: “Matatizo hayo yalitokea na yalishamalizwa. Kuhusu aliyefanya kitendo hicho, mwenyewe hajiwezi, akili zake si nzuri, lakini pia ni jeuri kila akiambiwa hasikii.”

Takwimu za ubakaji
Imebainika watoto 1,000 wanabakwa kila mwaka visiwani Zanzibar, kati yao 50 huripotiwa kufanyiwa vitendo hivyo kila mwezi.

Daktari wa Kituo cha Mkono kwa Mkono katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Dk Marijani Msafiri, anasema wengi ya watoto wanaofanyiwa udhalilishaji huo ni wenye umri chini ya miaka 16.

Anasema vitendo hivyo vinawasababishia watoto hao kushindwa kuendelea na masomo kutokana na kuathirika kiakili na kisaikolojia kwa kufikiria mara kwa mara walivyotendewa.

“Lengo la kuanzishwa Kituo cha Mkono kwa Mkono ni kutoa huduma kwa ajili ya kupata ushahidi utakaowatia hatiani watu wanaoshukiwa kufanya vitendo vya ubakaji dhidi ya watoto,” anasema Dk Marijani.

Mtandao wa Wanahabari Tanzania unaojumuisha watoto kutoka Unguja na Pemba, unalaani matukio ya ubakaji dhidi ya watoto ambayo yamekithiri Zanzibar.

Kwa mujibu wa takwimu za Jumuia ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (Zafela), matukio ya ukatili dhidi ya watoto ikiwamo ubakaji yaliyoripotiwa kwao katika mwaka 2014 ni 134.

Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulia na Idadi ya Watu (UNFPA), wamefanya utafiti katika Mkoa wa Kaskazini Unguja wa vitendo vya ubakaji watoto.

Utafiti uliofanywa katika kipindi cha Januari 2012 hadi Novemba 2013 ulithibitisha tatizo la ubakaji kwa mkoa huo ni ni kubwa kutokana na kesi 242 za kubakwa kuripotiwa katika maeneo tofauti.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto, vitendo vya ubakaji vimechukua asilimia 80 ya udhalilishaji wote unaofanywa Zanzibar.

Takwimu kutoka Kituo cha Mkono kwa Mkono, Kivunge zimeonyesha kwa kipindi cha Januari hadi Septemba 2013, wamepokea kesi 134 za udhalilishaji, kati ya hizo za ubakaji ni 81, sawa na asilimia 60 ya matukio yote ya udhalilishaji yanatokea mikoa ya Unguja.

Dawati la Jinsia Mkoa wa Kaskazini Unguja, limeripoti kesi 66 za ubakaji, Kituo cha Polisi Mahonda kimeripoti kesi 63 na Mahakama ya Mfenesini, imeripoti kesi 30 kwa kipindi cha mwaka 2012/2013.

Kati ya kesi 63 zilizoripotiwa Kituo cha Polisi Mahonda, kesi 31 ni zamwaka 2012 na 32 mwaka 2013.

Hata hivyo dawati hilo bado halina msaada wowote kwa waathirika wa ukatili wa jinsia kwa wanawake visiwani humo.

Utafiti huo umegundua vikwazo vinavyokwamisha kesi kupelekwa mahakamani ni pamoja na rushwa, muhali wa kifamilia, polisi kutoa uwamuzi kinyume na sheria na wazazi au walezi kutojua sheria ikiwemo kutunza ushahidi.

Ofisa Wanawake na Watoto Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Zuwena Hamad Omar anasema vitendo vya ubakaji mara nyingi hufanywa na walimu wa skuli, madrasa na ndugu wa karibu wa familia.

Anasema vikwazo vinavyochangia kesi za ubakaji kutofikishwa mahakamani ni rushwa iliyokithiri Jeshi la Polisi na mahakama.

Utafiti umebaini pia viongozi wa vijiji (masheha) baadhi yao wanachangia kuongezeka kwa ubakaji dhidi ya watoto wa kike na kulawiti wa kiume kwa kuficha taarifa wanazopelekewa au kuzisikia kwenye maeneo yao.