Mfalme wa Afrika Kusini aanza maisha jela

Mfalme wa kabila la Wathembu nchini Afrika Kusini ameanza kutumikia kifungo cha miaka 12 jela siku chache baada yake kupoteza rufaa.

Mfalme Buyelekhaya Dalindyebo alijiwasilisha mwenyewe kwa maafisa wa gereza.
Alihukumiwa kufungwa baada ya kupatikana na hatia ya kuteketeza mali, dhuluma na kuhujumu mfumo wa haki.

Mawakili wake walifika katika Mahakama Kuu jimbo la Eastern Cape katika juhudi za kumtaka aendelee kukaa nje kwa dhamana lakini ombi lao likatupiliwa mbali na mahakama na akatakiwa kulipia gharama.

Mwandishi wa BBC aliyeko Johannesburg Nomsa Maseko anasema mashtaka dhidi ya mfalme huyo yanahusu ukatili aliowatendea watu wa ufalme wake katika shamba alilomiliki jimbo la Eastern Cape miaka ya tisini.

Aliteketeza nyumba za wapangaji watatu kwa sababu alitaka kuwafukuza, akisema walivunja sheria za ufalme wake.

Aliwapiga wanaume watatu hadharani kwa madai ya kuenda makosa, AKijitetea, mfalme huyo aliambia mahakama kwamba aikuwa anawafunza adabu watu wa ufalme wake na haamini anafaa kuadhibiwa kwa kutekeleza wajibu wake.

Lakini jaji alimwambia kwamba hayuko juu ya sheria na akamhukumu kufungwa miaka 12 jela.