Mtazamo Muhimu Wa Kuanza Nao Mwaka 2016 Ili Uwe Wa Mafanikio Makubwa Kwako

Kila mwanzo wa mwaka watu wengi huwa wanaweka malengo, na malengo yanakuwa makubwa na mazuri sana. Lakini kadiri siku zinavyokwenda, watu wanaofanyia kazi malengo hayo wanazidi kupungua. Mpaka kufika mwisho wa mwaka, watu wanaokuwa wanafanyia kazi malengo wanakuwa wachache sana.

Mwaka huu, sisi wana mafanikio tumekuwa tofauti kidogo, badala ya kusubiri mwezi wa kwanza ambapo ndio kila mtu anaweka malengo, sisi tumeanza mwezi huu wa 12, na tumeuanza mwaka wetu mpya 2016 ukiwa na miezi 13. Kwa kufanya hivi kunakupa nafasi kubwa sana ya kuweza kuanza malengo yako kwa uhuru, kwa sababu mwezi huu wa 12 watu wengi hawafanyii tena kazi malengo waliyokuwa wameyaweka. Wachache wameyakamilisha na kuridhika na wengi wameshindwa kuyakamilisha na kukata tamaa.

Tukirudi kwenye sababu ya watu kuishia njiani wakati wa utekelezaji wa malengo, zipo sababu nyingi sana na kwenye makala hii; Sababu 10 Kwa Nini Hutafikia Malengo Yako 2015. nimezieleza vizuri, ibonyeze kusoma.

Leo nataka nikushirikishe kitu kingine muhimu sana ambacho kwenye makala hiyo sikugusia na huenda sikuwahi kukuambia kama ni muhimu pia kwenye kuweka malengo.

Ni hakika ya kwamba malengo mengi unayokwenda kuweka kwa mwaka 2016 ni malengo ya mabadiliko, kupata zaidi, kuwa zaidi na kwenda mbele zaidi. Lakini kutaka tu malengo yakubadilishe sio kitu rahisi, na hivyo kuna mabadiliko muhimu sana unayohitaji kufanya kabla hujapata mabadiliko ya malengo yako.

Kitu kikubwa ninachotaka kukushirikisha hapa ni kuanza mwaka 2016 ukiwa na mtazamo wa tofauti, mtazamo ambao utakuwezesha wewe kufikia malengo yoyote ambayo utakuwa umejiwekea. Na kuna mitizamo mingi sana unayohitaji kuwa nayo, ila kwa mwaka huu 2016 hakikisha unakwenda kwa mtizamo huu; KUTOA HUDUMA KWA WENGINE.

Amua kwa mwaka huu 2016 utakwenda kutoa huduma kwa wengine, na utakwenda kutoa huduma iliyo bora sana, ambayo mtu anayeipokea hajawahi kuipata sehemu nyingine yoyote.
Amua kwamba kile ambacho unakifanya, utajitoa kwa hali ya juu sana mwaka huu na kuhakikisha kila anayekutana na wewe, haondoki akiwa kama alivyokuja. Hakikisha anaondoka akiwa bora zaidi ya alivyokuja, akiwa na matumaini mazuri zaidi ya alivyokuja, na hakikisha anaondoka akiwa chanya zaidi ya alivyokuja.

Kama ambavyo wote tunavyojua, kama umekuwa msomaji wa makala hizi kwa muda, mafanikio yako wewe yapo kwenye mikono ya watu wengine. Ndio, hata ukikazana vipi, hutajiletea mafanikio yako wewe mwenyewe, bali watu ndio watakaokuletea wewe mafanikio. Kama unafanya biashara wateja wako ndio watakuletea wewe mafanikio, kama umeajiriwa, wale unaowahudumia ndio watakuletea wewe mafanikio.

Na hakuna mtu aliye tayari kukuletea wewe mafanikio kama huna mchango mkubwa kwenye maisha yao. Hakuna mtu atajitoa kukupa wewe mafanikio kama unachofanya kinaharibu maisha yao. Na itakuwa vigumu sana watu kukuletea mafanikio kama unachofanya wanaweza kukipata popote.
Ndio maana mwaka huu 2016, nakusihi sana wewe rafiki yangu, jipange kuwahudumia watu vizuri zaidi. Hii ni njia pekee, rahisi na ya uhakika kwako kuweza kufikia mafanikio makubwa. Kwa sababu kadiri wengi wanavyonufaika na kile unachowapatia, watasukumwa kuwaambia wengine wengi zaidi na hili litazidi kukusukuma.

Kwa wafanyabiashara. 
Kwa wafanyabiashara mwaka 2016 ni mwaka bora sana kwako, huu ni mwaka ambao wewe unakwenda kutoa huduma bora sana kwa wateja wako. Fikiria kutoa huduma zaidi, ndio unahitaji kupata faida, na ndio unahitaji kwenda mbele zaidi. Kama utaanza kwa kufikiri kutoa huduma bora sana kwa wateja wako, hayo ya faida na mafanikio wala hayatakuumiza kichwa, kwa sababu wateja wako wanaporidhika, wateja wako wanapopata huduma bora sana, hawa watawaleta wengine wengi zaidi na utaendelea kukua.

Pata muda ukae chini na itafakari sana biashara yako, iangalie biashara yako kama mteja na kama mshindani wako wa kibiashara. Ni kitu gani ambacho mteja anakikosa kwenye biashara yako, kijue vizuri sana. Pia jiulize ni kitu gani ambacho mshindani wako wa biashara naona hufanyi au hufanyi vizuri? Kijue na anza kufanyia kazi.

Kwa kuiangalia biashara yako kwa jicho la tofauti, utaona fursa nyingi sana na nzuri ambazo hukuwahi kuziona siku zote. Na mwaka huu 2016 zifanyie kazi fursa hizo, utashukuru sana baadae kwa jinsi ambavyo mambo yako yatakwenda vizuri.

Kwa walioajiriwa. 
Ufanye mwaka 2016 kuwa mwaka wa mapinduzi makubwa sana kwenye ajira yako. ufanye mwaka huu uwe mwaka wa wewe kutoa kile ambacho ni bora sana kwa mwajiri wako na hata wale wanaopokea unachofanya. Na hufanyi tu kwa sababu unataka kuwaridhisha wao, ila unafanya kwa sababu hiki ni kitu muhimu sana kwako kufanya.

Mwaka 2016 imiliki kazi yako, jiambie hii ni kazi yangu mimi, na chochote ninachofanya nataka kiwe na mhuri wangu, niwe tayari kukisimamia kifua mbele, mbele ya watu wengine. Usikubali kabisa kufanya kazi ya viwango vya kawaida, usikubali kabisa kusukuma tu siku ziende, amua kufanya kwa ubora wa kipekee.

Kaa chini na itafakari sana kazi yako, tafakari ni maeneo gani unayohitaji kuboresha. Ifikirie kazi yako kama yule mtu anayepokea unachofanya, je ungekuwa ni wewe ungependa iwe bora kiasi gani? Na pia tafakari kazi yako kama mwajiri wako, je kama wewe ungekuwa ndio mwajiri na umeajiri mfanyakazi kama wewe, ungetegemea nini kutoka kwake? Kwa kufanya zoezi hili makini sana, utaona fursa nyingi na nzuri za kuboresha zaidi kazi yako.

Kwa waliojiajiri. 
Kwa wale ambao wamejiajiri wenyewe, ambao wanatoa huduma ambazo zimekaa kibiashara na kiajira pia, kumbuka wewe ndio kila kitu. Mfanyabiashara anaweza kuweka watu wazuri na wakamsaidia kuuza bidhaa zake, ila kwa sisi tuliojiajiri hasa kwenye eneo la huduma, mambo sio rahisi sana.
Kumbuka wewe ndio kila kitu kwenye biashara yako, ina maana maamuzi unayofanya kwenye biashara hiyo au hata kwenye maisha yako, yanakwenda kuathiri moja kwa moja biashara yako. ni lazima ujue ya kwamba watu wamechagua kupata huduma yako, sio kwa sababu umewalazimisha, ila kwa sababu inawasaidia.

Mwaka 2016 hakikisha unakwenda kutoa huduma bora zaidi. Angalia wale wateja wako ni kipi ambacho wanahitaji, na kwa kuanzia kila mtu anahitaji kuwa na maisha bora, je wewe unawezaje kumsaidia kuwa na maisha bora? Njoo na njia bora sana kwa mtu kuweza kuwa na maisha bora na atakayoyafurahia. Fanya hivi na huduma yako itakwenda ngazi za juu zaidi kwa mwaka huu 2016.
Chukulia ni mwaka mmoja tu, wiki 52, siku 366.

Najua kadiri tunavyokwenda hapa kuna watu wanapata mawazo, ah kazi yenyewe imeshanichosha, siwezi kufanya hivyo. Au biashara yangu ni ngumu sana kufanya anachopendekeza. Na maneno mengine ya aina hiyo.

Nakuelewa vizuri sana rafiki yangu, huenda umeshakata tamaa sana na kazi unayofanya, unaona haiendi popote, labda kuna watu wanapendelewa, wewe unakazana lakini hakuna anayekujali. Labda biashara imekuwa ya kawaida sana, kila mtu anaifanya na hakuna mbinu zozote mpya unaweza kuja nazo, nakuelewa sana.

Lakini nakuomba kitu kimoja, fanya kitu tofauti kwa mwaka mmoja tu, mwaka huu mmoja tu 2016. Funga macho na masikio, futa kumbukumbu zote za nyuma, anza kama vile ndio siku yako ya kwanza kwenye kazi hiyo au biashara hiyo. Na fanya kwa mtazamo huu wa huduma, kila mara fikiria huduma gani bora sana unaweza kuwapa wengine, na tekeleza.

Ni kwa mwaka huo mmoja tu, kwa wiki 52 na siku 365. Unaweza kuhesabu hata kwa kushuka chini ili kuona ni siku ngapi zimepita. Halafu kama mwaka 2016 utaisha na hujaona mabadiliko yoyote kwenye maisha yako, basi unaweza kurudi kule ulipokuwa. Na kama unaona mabadiliko, unajua ni nini cha kufanya.

Ninachotaka kukusaidia wewe kama rafiki yangu hapa ni usiendelee kusema haiwezekani au kwa kazi/biashara yako hiko hakiwezekani, badala yake tenga mwaka huu kuhakikisha unatoa huduma bora sana kwa yule anayeitegemea kutoka kwako.

Na mwaka sio mrefu, umeshamaliza miaka mingi ambayo hukuwa na kikubwa cha kuangalia, kwa nini mwaka huu 2016 usiufanye wa tofauti?