SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA BARUA PEPE ZA KAWAIDA KATIKA MAWASILIANO YAKE

Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (kushoto) akipokelewa na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Bakari Jabiri leo alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala hiyo jijini Dar es salaam.

Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki (kulia) akitembelea maeneo mbalimbali ya Ofisi za Wakala ya Serikali Mtandao leo. Kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dkt. Bakari Jabiri leo alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala hiyo jijini Dar es salaam.


Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angella Kairuki akizungumza na Watendaji na baadhi ya Wafanyakazi wa Wakala ya Serikali Mtandao leo alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Wakala hiyo jijini Dar es salaam.

Serikali imepiga marufuku matumizi ya Barua pepe za kawaida kwa watumishi wa umma wanaotuma au kupokea taarifa za Serikali na kuwataka watumishi hao kuhakikisha kuwa wanatumia mfumo rasmi wa Mawasiliano ya Barua Pepe Serikalini (GMS) ulioanzishwa na Serikali kwa lengo la kuimarisha mawasiliano kwa njia ya Mtandao.

Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.Angella Kairuki alipokuwa akizungumza na Watendaji na Watumishi wa Wakala ya Serikali Mtandao ( e Government Agency) wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji na ufanisi wa matumizi ya TEHAMA Serikalini.

“Sasa kuna watumishi 7000 wanaotumia anwani za Barua pepe za Serikali ,idadi hii ni ndogo lazima iongezeke, hatuwezi kuendelea kuruhusu utumaji wa taarifa za Serikali kwa kutumia Barua Pepe nje ya mfumo huu” Amesisitiza na kuongeza kuwa Serikali haijakataza matumizi ya barua pepe za kawaida kwenye mawasiliano binafsi.

Amesema kwa kutambua umuhimu wa uimarishaji wa mawasiliano ya TEHAMA Serikalini na kuongezeka kwa matumizi ya TEHAMA katika utumaji wa taarifa kupitia mitandao mbalimbali ipo haja ya kuweka msisitizo kwa watumishi wa umma kutumia Barua Pepe za Serikali.

Mhe. Kairuki amewataka watendaji wa Wakala hiyo kuhakikisha kuwa wanasimamia uratibu wa zoezi hilo ili kuhakikisha kuwa Wizara, Idara na Taasisi zote za umma zinaunganishwa na mfumo rasmi wa Serikali ili kuwa na mfumo mmoja wa Mawasiliano.