FAIDA NYINGI ZA PAPAI

Mpapai ambao kitaalam hujulikana kama Carica papaya, ni mti wenye tunda lenye virutubisho vingi ambao una asili na hulimwa na kustawi katika nchi za kitropiki. Mpapai  hukua hadi kufikia kimo cha mita 10. Mti huu huwa na makovu ambayo hutokana na majani ya mpapai yaliyoanguka unapokua.

Mpapai ni wenye asili ya bara la Amerika ya kati na kusini lakini badae mmea wa tunda hili ulisambaa katika visiwa vya Caribbean, Florida na Baadhi ya nchi za Afrika. Leo hii papai hulimwa katika nchi za India, Australia, Indonesia, Philippines, Malaysia, U.S na Hawaii.

 Mmea huu wenye jinsia tatu: jike, dume na jikedume(hermaphrodite). Mpapai dume huzalisha poleni (mbegu dume) lakini hauzai matunda. Mpapai jike hauwezi kuzaa matunda bila kurutubishwa na poleni kutoka mpapai dume. Mpapai dumejike hujitegemea na waweza kuzaa matunda wenyewe. Na mipapai yote inayolimwa kibiashara huwa ni dumejike. Tunda la papai lina kirutubisho cha beta carotene ambacho hulipa papai rangi nzuri ya chungwa ya kung'aa.

Matumizi ya matunda na mboga za majani yamekuwa yakihusishwa na kupungua kwa athari za kiafya zisababishwazo na mfumo mpya wa maisha. Tafiti nyingi zimeonyesha kuwa kuongezeka kwa matumizi ya vyakula vitokanavyo na mimea kama papai hupunguza athari kama kuwa na uzito mkubwa, kisukari, magonjwa ya moyo na huboresha afya na kuongeza nishati mwilini.

Virutubisho katika papai
Jedwali likionyesha kiasi cha virutubisho katika gramu 100 za papai.
Aina ya kirutubisho
Kirutubisho
Kiwango kilichopo
Vitamini
Vitamini A
135ug

Vitamini E
1   ug

Vitamini C
62 mg

Thiamine
0.0mg

Niacini
0.3mg

Vitamini B 6
0.0mg

Folate
38 ug
Madini
Kalshamu
24mg

Phosphorasi
5 mg

Magnesiamu
10mg

Potasiamu
257mg

Munyu (Sodium)
3mg

Chuma
0.1mg

Zinki
0.1mg

Shaba
0.0mg

Manganizi
0.0mg
Protini muhimu
TRP(Tryptophan)
8mg

THR(Threonine)
11mg

ILE(Isoleucine)
8 mg

LEU(Leucine)
16mg

LYS(Lysine)
25mg

MET(Methionine)
2 mg

CYS(Cysteine)
5 mg

PHE(Phenylalanine)
9 mg

TYR(Tyrosine)
5mg

VAL(Valine)
10 mg
Tunda la papai lililowiva lina kiwango kikubwa cha Vitamini C (62mg) ukilinganisha na chungwa lenye kiwango cha 53mg katika gramu 100 za tunda. Tafiti zimeonyesha faida nyingi za vitamini C kama kuondoa sumu mwilini(sumu hizi hujulikana kama free radicals), kuimarisha kinga ya mwili na kujikinga na visababishi vya maumivu na uvimbe.

Papai hupunguza kiwango cha lehemu kwa kuwa lina Vitamini C na virutubisho vingine ambavyo huzuia kujijenga kwa lehemu katika mishipa ya damu ya ateri. Lehemu inapojikusanya kwa wingi katika ateri, mishipa hii ya damu huwa na njia nyembamba au kuziba na kusababisha kuongezeka shinikizo la damu na hata shambulizi la moyo.

Tunda hili husaidia kupunguza uzito wa mwili, papai lina fiba (nyuzi lishe) ambazo husaidia kupunguza uzito, unapokula tunda hili, fiba husababisha kujisikia umeshiba kwa hiyo mtu hupunguza kiasi cha chakula chenye nishati nyingi ambapo hupelekea kupunguza uzito wa mwili.

Afya njema ya macho hupatikana kwa kula tunda hili. Papai lina kiwango kikubwa cha Vitamini A na vitutubisho vingine kama Beta carotene ambavyo husaidia kuiweka katika hali ya afya njema ya ngozi utando ya macho, na kuzuia kudhurika kwa macho. Pia vitamini A huzuia kuharibika sehemu ya macho inayohusika na kuona kutokana na umri mkubwa na kutuepusha matatizo ya kuona.

Katika utafiti mmoja uliochapishwa katika jarida la magonjwa ya viungo(arthritis) ulionyesha kuwa, watu wanaokula vyakula vyenye kiwango kidogo cha vitamini C walikuwa katika hatari mara tatu zaidi ya kupata magonjwa ya viungo. Kula papai ni muhimu kwa afya ya mifupa yako kwa kuwa husaidia kuondoa visababishi vya uvimbe na maumivu pia lina vitamini C kwa wingi ambayo hutukinga na aina nyingi za magonjwa ya viungo.

Papai husaidia kuboresha mmeng'enyo, katika zama hizi, haikwepeki kula vyakula ambavyo huathiri mmeng'enyo na mfumo wa chakula. Mfano tunapokula vyakula vyenye mafuta na chumvi kwa wingi katika migahawa (junk food). Kula papai kutarekebisha mfumo kutokana na kuwepo kwa kimeng'enyo kijulikanacho kama papain pamoja na fiba kwa wingi ambazo husaidia kuboresha mmeng'enyo na kuimarisha afya yako.

Kuimarika kwa kinga ya mwili husaidia kujikinga na nyingi za magonjwa. Papai moja laweza kukuongezea kiasi kikubwa cha vitamini C inayohitajika mwilini kwa siku na vitamini hii inahusika katika kukutengenezea kinga imara mwilini.

Ingawa papai ni tamu, lakini lina kiwango kidogo cha sukari .Papai ni zuri kwa wale wenye kisukari kwa kuwa lina  vitamini na virutubisho ambavyo huwakinga wenye kisukari wasipate magonjwa ya moyo. Pia wasio na kisukari ni vyema kula papai ili kuweza kujiepusha na maradhi hayo yatishiayo maisha ya binadamu.

Wengi wetu hatupendi kuuzeeka, tungependa tuendelee kubaki katika hali ya ujana, lakini hakuna hata mmoja aliyefanikiwa. Papai hupunguza kasi ya kuzeeka kwa uwepo wa Vitamini C kwa wingi, viondoa sumu(antioxidants) pia kirutubisho cha beta carotene ambavyo hulinda ngozi zetu dhidi ya sumu (free radical) ambazo husababisha makunyanzi ya ngozi na hali nyingine za kuzeeka.

Mbali na kuiweka ngozi katika hali ya afya njema, papai pia husaidia ukuaji wa njwele na kuwa zenye afya, Vitamini A husaidia katika utengenezaji wa Sebum, kemikali ya kibiolojia ambayo huzifanya nywele zetu kuwa nyororo, imara na za kung'aa. Virutubisho katika tunda hili huzuia pia kunyonyoka kwa nywele.Mbali na kusaidia katika ukuaji wa nywele imara, inadhaniwa kuwa papai husaidia pia kuzuia nywele zisiwe nyembamba na kuzuia kukatika.

Uwepo wa viondoa sumu katika papai, husaidia kutukinga na maradhi ya saratani. Katika utafiti mmoja uliofanyika katika chuo kikuu cha Harvard katika kitivo cha afya ulionyesha kuwa, beta carotene katika papai huzuia kukua kwa saratani ya tezi dume na saratani ya utumbo mkubwa.

Mbali na vitamini na protini muhimu zilizopo katika tunda hili, pia kuna aina tofauti za madini(tazama jedwali) muhimu yanayohitajika mwilini kufanya na kurekebisha kazi mbalimbali za mwili. Faida nyinginezo mbali na tulizoziona awali za ulaji wa papai ni pamoja kuondoa msongo wa mawazo, kusaidia kupunguza maumivu ya hedhi, kupunguza hatari ya kupata pumu na husaidia ngozi au majeraha kupona haraka.