Magufuli, Malinzi wampongeza Samatta

Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli amempongeza nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta kwa kusajiliwa na klabu ya KRC Genk inayocheza Ligi Kuu  Ubelgiji.

Katika salamu hizo alizotoa kupitia kwa Waziri wa Michezo, Nape Nnauye, Rais amesema mchezaji huyo ameijengea heshima na kuitangaza Tanzania kimataifa.

“Mafanikio ya Samatta kucheza katika ligi kubwa duniani, yanafungua milango ya wanasoka wengine wa Tanzania kujiunga na timu kubwa duniani, ambako licha ya kujipatia ajira zenye kipato kizuri, kunaiwezesha kuinua soka lake,” amesema Rais Magufuli.

Alisema amefurahishwa na mafanikio anayoendelea kuyapata mshambuliaji huyo na kuwataka wanasoka wengine kuyachukulia kama changamoto ya kufanya vizuri.

Aidha, Rais Magufuli amemtaka Samatta kuongeza juhudi akiwa kwenye timu yake mpya ya KRC Genk, na kumuombea mafanikio.

Wakati huohuo; Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamal Malinzi amempongeza Samatta kwa kufanikiwa kujiunga na klabu ya Racing Genk.

 Malinzi amempongeza Samatta kwa kupata nafasi ya kucheza Ligi Kuu Ubeligiji baada ya kusaini mkataba wa miaka mitatu na nusu kuichezea RC Genk.

Malinzi amemtaka Samatta kujituma kwa nguvu zake zote na uwezo wake wote ili kuendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania katika nyanja za kimataifa na kwa sasa barani Ulaya.

 Aidha Malinzi amewataka wachezaji wengine kujituma na kutumia nafasi wanazozipata katika klabu zao kwa kufanya vizuri na kupata nafasi ya kuvuka kwenda kucheza soka la kimataifa nje ya nchi. Kabla ya kujiunga na KRC Genk, Samatta alikuwa mchezaji wa TP Mazembe ya DR Congo na msimu uliopita alifanikiwa kutwaa ubingwa