Mahakama inampango wa kuangalia upya masharti ya dhamana kwa wafungwa

Jaji mkuu Mheshimiwa Othuman Chande amesema idara ya mahakama iko katika mchakato wa kuangalia upya masharti ya dhamana yanatolewa katika mahakama za mwanzo baada ya kubainika kuwa ni magumu na yanachangia mlundikano wa mahabusu katika magereza yote nchni.

Akizungumza katika uzunduzi wa wiki ya elimu ya sheria nchni uliofanyika katika viwanja vya mnazi mmoja, Mhe. Chande amesema sharti la dhamana sio adhabu kwa mtuhumiwa na kusisitiza tayari mahakimu katika ngazi ya mahakama za mwanzo, wilaya na mikoa wameenza magerezani kuzungumza na mahabusu ili kubaini matatizo yao na kubaini moja ya changamoto kubwa ni masharti magumu ya dhamana.

Aidha katika uzinduzi huo idara ya mahakama imesema inaangalia uwezekano wa kutoa adhabu mbadala kwa wafungwa waliohukumiwa kifungo cha chini ya miaka mitatu ikiwemo vifungo vya nje kwa kufanya kazi za kijamii zinazosimamiwa idara ya ustawi wa jamii kwa kuwa inakubalika kisheria na itasaidia kupunguza msongamano wa wafungwa magerezani.

Awali akizindua wiki hiyo kwa niaba ya rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Bwana Saidi Mecky Sadiki ametaka utaratibu wa maazimisho ya wiki ya sheria wa kutoa elimu ya maswala ya kisheria usogezwe kwa wananchi zaidi hususani waishio vijijini kupitia mahakama za mwanzo,wilaya ili kuwawezesha kuelewa haki na stahiki zao.

Taasisi mbalimbali zinazosimamia haki na sheria zimepanga kutoa elimu sheria kwa wananchi kwa siku tatu mfululizo katika viwanja vya mnazi mmoja ili kuwajengea wananchi uwezo.