NJIA RAHISI ZA KUDHIBITI ‘STRESS’ ILI KUEPUKA SHINIKIZO LA DAMU

Mwanadamu anakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile za kiuchumi, kiafya na kijamii.  Changamoto zote hizo huongezeka pindi mwanadamu anapofikia umri wa utu uzima, kwa maana ya kubebeshwa majukumu ya kimaisha, kama vile kusaidia wanafamilia, wanaukoo na jamii kiujumla.

Hata hivyo, changamoto kubwa za kiafya zinazomkabili mwanadamu huyu, karibu kote ulimwenguni ni ugonjwa wa mkazo, ambao umezoeleka kwa wengi kama ‘stress’ ambazo zinaweza kumfanya mtu kupatwa na shinikizo la damu.

Baadhi ya vitu vinavyosababisha ugonjwa huu wa mkazo kwa mujibu wa wataalamu wa afya ni hofu au wasiwasi, kuhusiana na jambo lolote linaloweza kumkumba mwanadamu, hasa ukosefu wa fedha au kutamani utajiri ambao hajui ataupataje.

Pia, ratiba za shughuli za kiuchumi na huduma zenye mambo mengi yasiyokuwa na mpangilio huweza kumsababisha ugonjwa huo mwanadamu.  Jambo jingine ni ugomvi usiokwisha ndani ya familia, kukumbana na matukio ya kutisha kama vile ya ugaidi na kadhalika.

Watu wengi ulimwenguni wamezoea kutumia kilevi, kama vile pombe, tumbaku na vileo vingine ili kukabiliana na maradhi hayo ya mkazo na kupanda kwa shinikizo la damu.

Hali hiyo, inatokana na wengi wao hao kushindwa hata kula vizuri, huku baadhi yao wakilazimika kutumia muda mwingi kuangalia matukio katika televisheni au kutumia vifaa vya kielektroniki kama vile kompyuta na simu za mkononi kwa muda mrefu ili kujisahaulisha na msongo wa mawazo kichwani.

Mkazo na kupanda kwa shinikizo la damu, ni vitu vinavyoendana katika maisha ya binadamu.  Ndiyo maana ili kudhibiti magonjwa hayo, mhusika hushauriwa kwanza kudhibiti hali yake ya mkazo.  Kituo kimoja cha matibabu ya akili kilichopo nchini Uingereza, kinaeleza kwamba katika kila kundi la watu watano ulimwenguni, mtu mmoja hukumbwa na maradhi ya mkazo, yanayotokana na mazingira ya mahali pake pa kazi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, kushindwa kukabiliana na hali hiyo ya mkazo mwingi, mtu mmoja kati ya watu wanne, hujikuta akilia peke yake bila kupigwa wala kukasirishwa na yeyote, akiwa kazini kwake.

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba mwanadamu ameumbwa kwa njia ya kipekee kabisa, kwa kuwekewa mifumo mbalimbali mwilini inayofanya kazi mbalimbali usiku na mchana ili tu kumweka vizuri na salama katika maisha yake.

Kwa mfano, mwanadamu amewekewa mfumo wa hisia za dharura, ambao ni kichocheo kikuu cha mwili pindi mwanadamu huyu anapopatwa na mkazo mwingi.

Vichocheo hivyo, ndivyo vinavyomfanya binadamu huyo anapopatwa na hali hiyo aweze kupumua haraka, moyo wake uende mbio na hali inayochangia kuongezeka kwa shinikizo la damu.  Vichocheo hivyo, ndivyo huongeza chembe za damu na sukari kwenye damu.

Kwa kawaida, mfumo huo wa hisia za dharura unafanya kazi kubwa ya kumtayarisha mwanadamu kukabiliana na kitu chochote au mtu yeyote anayemsababishia hali hiyo ya mkazo.

Hata hivyo, baada ya jambo hilo linalosababisha mkazo kupita, mwili hurudi katika hali yake ya kawaida, ingawa baadhi ya wataalamu wanaweka wazi kuwa endapo hali ya hisia za dharura inajirudia mara kwa mara, mtu anaweza akakumbwa na ugonjwa mwingine wa hofu au wasiwasi, ambao kitaalamu unajulikana kama ‘Anxiety Disorder’.

Kwa hiyo, kwa kila binadamu ni muhimu kujifunza mbinu za kukabiliana na maradhi hayo ya mkazo na kupanda kwa shinikizo la damu.

Njia 10 kuepuka ‘stress’
Kwa sasa zipo njia kuu rahisi 10 za kukabiliana na hali hiyo: 

1.  ni kuhakikisha unapata muda wa kutosha wa kulala usingizi.  Kutopata usingizi wa kutosha kunaathiri hisia, akili, kiwango cha nishati mwilini pamoja na afya kwa ujumla.  Wataalamu wa afya wanashauri mtu mzima apate usingizi wa walau saa nane katika masaa 24 za siku.

2.  katika kujipangia mipango ya maisha, unashauriwa kutanguliza mambo muhimu yanayokuwezesha kuishi kwa kula kwa kiasi.

Kwa maneno mengine, binadamu anatakiwa kufikiri jinsi ya kurahisisha maisha yake, pengine kwa kupunguza gharama za maisha pamoja na kupunguza muda anaotumia kazini kwake.

3.  jifunze mbinu za kupumzisha mwili.  Kutafakari kwa kina, mazoezi ya kuvuta pumzi na yoga ni njia imara za kuondoa mkazo.

4.  mtu inampasa kuimarisha mtandao wake wa kijamii.  Kujiunga na vikundi mbalimbali kama vile vya masomo, kutoa misaada kama vile kwa watoto, yatima na wajane au vikundi vya wajasiriamali.

Mwaka 2008, baadhi ya watafiti raia wa Uingereza waligundua njia moja ya kubaki imara pindi mtu anapopatwa na mkazo.  Katika utafiti wao, wanasema moja ya njia ya kubaki imara, ni kujitolea kuwasaidia wengine kwa njia fulanifulani.

5.  mtu inampasa kuelewa vizuri hisia za wengine, kitu kitakachosaidia kupunguza hasira, na wakati huohuo awe mwepesi kusamehe kwa kuwa ni jambo jema pia kimaisha.

Utafiti uliofanywa mwaka 2001 nchini Uingereza, ulionyesha kuwa mtu anapokuwa na kinyongo fulani kwa mtu, humsababishia kupanda kwa shinikizo la damu pamoja na kuongezeka kwa mapigo ya moyo.  Hali hiyo, kwa mujibu wa utafiti huo, inaweza kuondolewa kwa mtu kuwa mwepesi wa kusamehe haraka.

6. kwa gharama yoyote, mtu anatakiwa kujiepusha na ugomvi wa aina yoyote ile.  Kugombana na wengine kunaweza kumletea au kumsababishia mtu mkazo mwingi.  Mtu anapokuchokoza, jitahidi kutulia, usimwage ugali kwa kuwa yeye kamwaga mboga.  Inashauriwa kujitenga naye kwa kukaa faragha, hivyo kusuruhisha mambo kwa hekima na busara nyingi.

7.  jipangie ratiba ya matumizi ya muda kwa kuandaa muda wa kutatua matatizo ya familia na ya kazini, kwa kutumia mbinu bora za makubaliano.  Aidha, mtu anaweza akatunza muda wake wa kazi na familia kwa ufanisi, hivyo kupunguza kiwango cha mkazo kwake.

8. inampasa mtu ajitahidi kupunguza hali zitakazomwongezea mkazo kadri awezavyo, kwa kutoruhusu hali za kuongeza mkazo.  Kwa mfano, kujiepusha kuwaza mambo mabaya yanayoweza kutokea na kuchota hisia zake.

9. ni kuhakikisha mwili mzima unatunzwa.  Baada ya kazi nzito, jitahidi kuukanda mwili kwa maji ya uvuguvugu, kabla ya kula chakula.  Mazoezi ya kutembea na kusikiliza muziki ni muhimu kwa sababu unaifurahisha nafsi yako.

10.  ni kuondokana na woga wa kuomba msaada kwa jamaa na marafiki au majirani.  Baadhi ya tafiti zinaonyesha kwamba kuzungumza na marafiki au watu wa familia kuhusu hali inayokupata, husaidia kuondoa ugonjwa wa mkazo.  Inashauriwa endapo mkazo na hali ya wasiwasi itaendelea, ni muhimu kutafuta msaada zaidi kwa daktari.