SIRI KUBWA YA KUTIMIZA MIPANGO YAKO MAISHANI

Mwezi huu ni mwezi ambao tutakuwa tunatoa makala nyingi kwa ajili ya kuelimisha wale ambao wanapenda kutimiza ndoto zao na malengo yao katika maisha. Tunaamini kila mtu ana malengo yake katika maisha. Kila mtu ana ndoto na mpango anaopenda uende sawa. Ni kama ramani ya hali na mazingira unayopenda kuwepo na kuyaishi katika muda/wakati ujao. Malengo na ndoto zako ni sawa na nchi yako ya Ahadi. Nchi ya Asali na Maziwa, nchi ya Matunda na nafaka. Hivyo ni vyema kutafakari na kutumia muda huu kujaribu kuelekeza jinsi na namna mbalimbali ambazo tunaweza kufika katika nchi hiyo ya ahadi.

Leo tutapenda kuzungumzia, kuhusu muda na nguvu kazi unayoitumia katika kutimiza malengo yako. Je muda huu unautumia kivipi katika kufikisha malengo yako? Je wakati huu unautumia kivipi katika kutimiza malengo yako? Time is precious.

Ukiwa unatenda jambo lolote, jiulize na tafakari. Je ninachotenda kina umuhimu gani katika maisha yangu? Je kitanifanikishia mimi kufika malengo yangu? Tazama faida na hasara za kila kitu. Tazama kila jambo utendalo kiundani na kwa kutumia akili zako vyema. Jambo unalolitenda lina matokeo katika maisha yako. Ni vyema kuyatambua matokeo ya kila jambo na kisha yalinganishe na malengo yako.

Mfano, kama una malengo ya kuwa na afya njema na kuishi maisha marefu. Tazama wakati huu wa sasa unautumia kivipi kutimiza malengo hayo? Je umetenda nini leo kutimiza malengo yako? Kama  ukitambua hayo, utajitahidi kutumia wakati wako na nguvu yako kufanya jambo litakalopelekea kutimiza malengo yako. Utaacha kula vyakula vyenye madhara mwilini, mfano Chipsi mayai ya kisasa, utapunguza vyakula vya mafuta, utaacha kula kwa kuridhisha mdomo bali utakuwa unakula kwa malengo ya kiafya zaidi. Kama kuna matendo ambayo yana madhara kwenye afya yako nayo utayakabili na kubadilika. Kama ni mtumiaji wa madawa ya kulevya unaacha, kama ni mtumiaji wa tumbaku na sigara utaacha, kama ni mlevi kupindukia utaanza kuijali afya yako kwa kuacha au kupunguza pombe. Vyote hivi mwishoni utaona unatimiza malengo yako. Taratibu taratibu utaona umebadilika na kufikia malengo yako.

Kama una malengo ya kuwa na kazi nzuri, basi ni vyema kutumia wakati wako huu hata kwa kidogo kidogo. Utaanza kuacha uvivu na kujituma katika mambo yako, wasiliana na watu unaowajua wanaoweza kukusaidia kutimiza malengo yako, kama ni kusoma kwa bidii itakubidi usome kwa bidii ili ikusaidia katika soko la ajira, utakuwa mtu wa kujituma na kutumia mipango yoyote kufanikisha malengo yako.

Kama unapanga kupata mke/mme bora basi utaanza kutenda yaliyosahihi ambayo yatakusaidia kutimiza ndoto yako. Mfano utaanza kujipenda na kujithamini kwanza, utakuwa mwaminifu na kujifunza kutokuwa mtu wa zinaa. Shirikiana na watu mbalimbali ukutane na watu mbalimba kwa utapata marafiki wapya na mwisho unaweza kupata mke/mme ambaye hukutegemea au ambaye uliona ni vigumu kumpata. Pia utajiheshimu kwani kama unapenda uwe na mke au mme bora, jiandae kwanza kuwa mke au mme bora kwanza.

Hivyo Unautumia wakati huu kufanya nini? Andika list ya mipango yako ya baadaye na kisha ifanyie kazi kila siku taratibu taratibu na kisha utajikuta umeweza kufanikisha mipango yako.