Viongozi wa dini na watanzania wasikitishwa na mwenendo wa bunge

Mkuu wa kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) askofu Dk Fredrick Shoo amemweleza waziri mkuu Mh. Kasimu Majaliwa kuwa viongozi wa dini na watanzania wanasitishwa na hali inayoendelea katika bunge la kumi na moja ikiwamo vurugu ambazo siku chache zilizopita zilisababisha baadhi ya wabunge kutolewa kwa nguvu nje ya ukumbi wa bunge na askari wa jeshi la polisi.

Akizungumza muda mfupi baada ya kuingizwa rasmi kazini kama mkuu wa kanisa la KKKT, askofu Dk Fredrick shoo amewataka wabunge kuheshimu na kuitunza heshima ya bunge kwa kuwa bunge ni nyumba ya demokrasia na inahitaji iheshimiwe.

Dk Shoo amewataka wabunge kuwa na nidhamu na kwamba watanzania wanatarajia kuona na kusikiliza hoja zinazojadiliwa katika bunge la jamuhuri ya muungano wa Tanzania kwa uwazi katika hali ya kistaraabu.

Awali akiongoza ibada maalumu ya kumuingiza kazini mkuu wa kanisa hilo Dk Fredrick Shoo aliyekuwa mkuu wa kanisa kwa miaka minane iliyopita askofu Dk Alex Malasusa amewataka watanzania kumwombea kiongozi huyo ili aweze kufanya kazi ya kuliongoza kanisa hilo kwa uadilifu.

Waziri mkuu wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Mh.Kassim Majaliwa amesema serikali itahakikisha inasimamia kwa dhati mwenendo mzima wa bunge ili kuondoa kasoro ambazo zimekuwa zikijitokeza ndani ya bunge hilo na kusababisha kero kwa watanzania.

Akitoa salamu za umoja wa makanisa mkoani Kilimanjaro askofu wa kanisa katoliki jimbo la Moshi askofu Isac Aman amewataka watanzania kuwa na uzalendo katika kufanya kazi kwa bidii ili kuwezesha serikali kupata fedha za utekekelzaji wa miradi ya maendeleo.

Ibada ya kumuingiza kazini mkuu wa kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania KKKT iliyofanyika katika usharika wa Moshi mjini imehudhuruwa na viongozi mbalimbali wa dini wabunge ikiwemo aliyekuwa mgombea uraisi wa vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi UKAWA Mh. Edward Lowassa, waziri mkuu mstaafu Mh Fredrick Sumaye na mwenyekiti wa makampuni ya IPP Dk Reginald Mengi.