Bao la Kakolanya lawa gumzo Mbeya


Wachezaji wa Prisons. Wa mbele ni kipa Beno Kakolanya. 

Mbeya. Bao la pili alilofunga kipa wa Tanzania Prisons, Beno Kakolanya katika ushindi wao wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City katika Kombe la Shirikisho (FA), limezuia gumzo katika mitaa ya Jiji la Mbeya.

Kipa huyo aliupiga mpira kwa guu la kulia wakati timu hizo zikiwa sare ya 1-1  katika dakika ya 82  na kusababisha bao lililoiwezesha Prisons kutinga robo fainali ya Kombe la FA. Kakolanya, akiwa eneo la goli lake aliupiga mpira mrefu uliowapita wachezaji wote 20 wa kati  na hatimaye kudunda mbele ya golikipa wa Mbeya City, Haningtong Kalyesubulana na kuruka juu kwenda kutua ndani ya nyavu.

Bao hilo liliamsha mshangao kwa wapenzi wa soka wakiwamo wachambuzi wa soka ambao walisema sasa atakuwa kipa wa pili nchini kufunga bao la aina hiyo. Walisema kipa wa kwanza kufunga bao kama hilo alikuwa Juma Kaseja, ambaye aliifunga timu ya Toto Afrika Mwanza wakati akiichezea Yanga wakati ilitoka sare ya mabao3-3 kwenye Uwanja wa CCM  Kirumba Mwanza. Kakolanya aliliambia gazeti hili kwamba hakutegemea kufunga bao hilo na ni mara ya kwanza kufunga bao kama lile tangu aanze kucheza mpira.

‘’Imenishangaza kidogo, lakini kumbe mpira ndivyo ulivyo kwamba lolote linaweza kutokea, nimefurahi kwani nimeivusha timu yangu kwa bao la pili na kwa sasa tutajipanga kwa hatua nyingine iliyo mbele yetu,” alisema Kakolanya.

Mchezo wa Mbeya City na Prisons ulitanguliwa na vituko vingi vikiwamo vya watu kuchoma mayai alfajiri kwenye milango ya uwanja.

 0  0 0  0  0