Bodi ya ERB yawafutia usajili wahandisi 330

Mwanza. Bodi ya Usajili wa Wahandisi Tanzania (ERB), imewafutia usajili wahandisi 330 na kampuni 37 kwa sababu ya utovu wa nidhamu, kukiuka maadili na  kuisababishia Serikali hasara na wateja wengine.

Hayo yalisemwa na Msajili wa ERB, Steven Mlote wakati wa kuwaapisha wahandisi wataalamu na washauri wa vitengo tofauti vya jijini Mwanza juzi.

Alisema leseni za wahandisi na kampuni hizo zilifutwa kati ya mwaka 2005 hadi mwaka huu.

Miongoni mwa wahandisi na kampuni za ujenzi zilizofutiwa leseni mwaka huu ni pamoja na Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Reuben Muyungu na Mhandisi Mshauri, Heri Sanga ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya  Nimeta Consult Ltd.

Walijenga chini ya kiwango barabara ya lami ya kilomita 4.5 kwa iliyopo Bariadi Mjini kwa gharama ya zaidi ya Sh9.1 bilioni.

Alisema tayari Serikali imewasimamisha kazi pia watumishi kadhaa wanaodaiwa kuhusiana na kitendo hicho.

Akizungumza wakati wa kuwaapisha wahandisi 20 waliokabidhiwa leseni za uhandisi, Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Mkoa ya Mwanza, Yusto Ruboroga aliwaasa wahandisi kutunza viapo vyao na kuwaonya kuwa ni kosa la jinai kwa yeyote kuvikiuka.

“Kiapo ni tamko la kisheria, utaratibu wa kuwaapisha wahandisi washauri na wataalamu ni kwa mujibu wa Sheria ya Viapo ya mwaka 2002 Sura ya 34 na Sheria ya Usajili wa Wahandisi Namba 15 ya 1997 pamoja na marekebisho yake ya 2007. Kila anayeapa anajifunga mwenyewe kwa kiapo chake,” alisema Ruboroga.

Mmoja wa wahandisi walioapishwa, Jinati Hamduni alisema taaluma ya uhandisi inakumbana na changamoto kadhaa ikiwamo ya kuvamiwa na watu wasio na sifa na baadhi yao kushindwa kuweka mbele masilahi ya Taifa wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Tangu utaratibu wa kuwaapisha wahandisi uanzishwe mwaka 2013, bodi hiyo tayari imewaapisha wahandisi 2,110 kati ya wahandisi 16,032 waliosajiliwa.

Tanzania pia ina jumla ya kampuni za ushauri 283 zilizosajiliwa.