Bunge la Afrika Mashariki lampongeza Rais Magufuli

Bunge la Afrika Mashariki limempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya ya kuhakikisha mapato ya nchi yanakusanywa kikamilifu na yanawanufaisha wananchi wote.

Akiongea kwa niaba ya wabunge hao mbunge Shyrose Bhanji amesema kuwa eneo kubwa ambalo Rais amehakikisha linasimamiwa vizuri ni eneo la bandari eneo ambalo limerudisha heshima na uaminifu kwa wafanyabiashara kutumia bandari ya Tanzania na hivyo kuongeza mapato ya nchi.

Mheshimiwa Banji ameongeza kuwa nchi zote za Afrika Mashariki zinaitegemea sana bandari ya Dar es salaam hivyo nchi wanachama wa Afrika Mashariki wamekuwa na furaha kubwa kuona kuwa bandari hiyo imepiga hatua na wana uhakika kuwa bandari hiyo itarahisisha biashara kwa wafanyabiashara wa ukanda huo.