Kapombe mchezaji bora wa Januari


Shomari Kapombe (kulia)

Dar es Salaam. Beki wa Azam, Shomari Kapombe ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom ya Januari 2016.

Katika mwezi huo uliokuwa na raundi tatu, Kapombe alicheza dakika zote 180 za mechi mbili za timu yake dhidi ya African Sports na Mgambo Shooting.

Mechi ya tatu ya Azam FC katika raundi hiyo dhidi ya Tanzania Prisons ilikuwa kiporo na ilichezwa Februari 24, 2016.

Kapombe alifunga mabao yote mawili kwenye ushindi wa mabao 2-1 wa timu yake dhidi ya Mgambo Shooting. Pia, alisaidia kupatikana bao la Azam kwenye mechi dhidi ya African Sports iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1, na mara nyingi mashambulizi ya timu yake yalianzia upande wake.

Washindani wa Kapombe kwenye kinyang’anyiro hicho kwa mwezi huo walikuwa mshambuliaji wa Tanzania Prisons ya Mbeya, Jeremiah Juma na beki wa Coastal Union ya Tanga, Miraji Adam.

Kwa kutwaa tuzo hiyo, Kapombe atazawadiwa Sh1 milioni  na wadhamini wa ligi hiyo, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom Tanzania Limited.

 0  0 0  0  0  0