Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe
Mbali na kuponda mpango huo, ameishauri serikali kurudi nyuma na kujitafakari kabla ya kuendelea kuutekeleza.
Bashe aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa Twaweza wenye jina la Mwanga Mpaya? ambayo ililenga kukusanya maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko kwenye sekta ya elimu, ikiwamo kuanza kwa mpango wa elimu bure kuanzia elimu ya msingi mpaka sekondari.
“As a nation we are in a crisis (kama nchi tuko kwenye wakati mgumu).
Si dhambi kukiri tulifanya kosa katika kuutekeleza mfumo huu wa elimu bure na hatujui tunataka kujenga taifa la namna gani kwa sababu tulishafanya makosa awali. Tunapaswa kukaa mezani na kuanza upya,” alisema.Alisema serikali inachokitoa kwa wananchi si elimu bure bali wananchi wanachangia kupitia kodi zao wanazotozwa na serikali.
Mbunge huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, ambayo inasimamia pia sekta ya elimu, alisema kwa sasa serikali haifahamu inataka kujenga taifa la namna gani kwa kuwa makosa yalishafanyika miaka ya nyuma katika sekta hiyo.
Bashe alisema nchi kwa sasa iko katika matatizo makubwa ya mfumo wa utoaji wa elimu na serikali haikujipanga vizuri katika kuuanzisha.
“Tanzania isione aibu kurudi nyuma na kuutafakari mfumo wa elimu. Kuna nchi nyingi duniani ziliwahi kufanya hivyo kwa mfano Marekani mwaka 1991,” alisema Bashe.
Alisema elimu bure inayotolewa sasa haiendani na mazingira halisi ya wananchi kwa kuwa shule nyingi bado ziko katika wakati mgumu kwa kukosa madawati na vitabu.
Bashe alisema tangu mwaka 2006, mawaziri waliokuwa wanaongoza sekta ya elimu walikuwa wanakuja na mikakati ambayo haikuwa na lengo la kuikomboa elimu ya taifa wala kuangalia upimaji wa mafanikio.
Alisema tangu nchi ipate uhuru, idadi ya wanafunzi wanaoanza elimu ya msingi imekuwa ikiongezeka, huku baadeye ikipungua kutokana na mitihani ya mchujo (darasa la saba, kidato cha nne) na wengi wao kuishia mitaani wakiwa hawana shughuli maalumu.
Alisema sera ya elimu iliyozinduliwa mwaka 2014 haiinui ubora wa elimu nchini, hivyo serikali inapaswa kurudi mezani na kujipanga upya katika kuitekeleza.
Alisema umasikini nchini hauwezi kuondoka bila kuwekeza katika elimu na kwamba hata uanzishwaji wa viwanda utashindwa bila wananchi kuwa na elimu ya kuendesha viwanda hivyo.
“Mimi natoka Nzega kuna shule walimu wanalala darasani, wanafunga godoro na neti madarasani, wanalala pindi wanafunzi wanapoondoka kwenda nyumani. Ikifika asubuhi wanaondoka vifaa vyao,” alisema Bashe.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule Kuu ya Elimu, Dk. Joviter Katabaro, alisema nchi kwa sasa iko vitani kielimu. Alisema serikali inatakiwa kujipanga vizuri kuhakikisha mfumo wa elimu unamjega mwanafunzi kimazingira.
Alisema mfumo wa elimu ya Tanzania unatengeneza wanafunzi wasiojua kusoma wala kuandika. Pia alisema Alisema mfumo wa elimu nchini haumjengi mwanafunzi aliyemaliza ama darasa la saba, kidato cha nne, cha sita au chuo kikuu kuwa na uwezo wa kujitegemea.
UFAULU USIO NA TIJA
Alisema zamani shule zilikuwa zinafaulisha mwanafunzi mmoja hadi wawili kwa sababu hakukuwa na shule za kutosha za kupokea wanafunzi, lakini kwa sasa kuna shule nyingi za kata, hivyo idadi kubwa ya wanafunzi wanafaulu bila kuwa na uwezo kwa sababu shule ni nyingi.
“Rais Magufuli ameanzisha mpango wa elimu bure kwa nia njema lakini washauri wake wa elimu hawajafanya utafiti wa kutosha kubaini ni vipengele gani vipewe kipaumbele,” alisema Dk. Katabaro.
SHULE BINAFSI
Alisema kuongezeka ka shule binafsi nchini kumetengeneza matabaka, akitolea mfano matokeo ya kidato cha nne yaliyotolewa huivi karibuni kwa shule binafsi kuongoza na shule za serikali kushika mkia.
Alisema Waziri mwenye dhamana ya elimu anapaswa kuangalia suala la uwapo wa shule binafsi kwa sababu unatengeneza matabaka ambayo yatasababisha athari kubwa miaka ijayo.
Alisema wanafunzi wa shule za serikali wanashindwa kufaulu kwa sababu mazingira yao ya kusomea ni mabovu.
Dk. Katabaro alisema kutokuwapo kwa bodi ya walimu kunachangia kuwapo kwa ufaulu mbovu wa wanafunzi nchini, akitolea mfano wa bodi za madaktari, wahandisi, wahasibu na wanasheria.
“Walimu wanapenda kazi yao kwa kuwa taaluma yao ina wateja wengi, lakini mfumo wa elimu nchini ni mbovu na unapaswa kusukwa upya,” alisema Dk. Katabaro
RIPOTI YA TWAWEZA
Ripoti ya Twaweza inaonyesha asilimia 88 ya wananchi waliohojiwa, wanaamini elimu bure itatekelezwa katika muda uliopangwa na asilimia 76 wanaamini sera hiyo itasaidia kuwa na elimu bora zaidi.
Asilimia 15 ya watu wengine walisema elimu bure haitaboresha elimu wakiamini ongezeko la udahili wa wanafunzi, hauendani na rasilimali zilizopo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Twaweza, utafiti huo ulifanywa kati ya Desemba 10, mwaka jana na Januari 2, mwaka huu. Watu 1,894 kutoka Tanzania Bara walihojiwa.
Utafiti huo ulibaini kwamba wazazi walikuwa wanaelemewa na michango ya shule. Asilimia 89 ya wazazi wanadai walikuwa wakilipa michango mbalimbali, kati yao asilimia 80 walisema walikuwa wakilipa mpaka Sh. 50,000 kwa mwaka, asilimia nane wakilipa zaidi ya Sh. 100,000 kwa mwaka.
Kati ya waliohojiwa, asilimia 49 wanaamini michango yao haitumiki ipasavyo na asilimia 58 wanasema michango hiyo haijaidhinishwa na serikali. Aidha, asilimia 89 ya waliohojiwa kwa njia ya simu, walisema walimu hutumia michango waliyokuwa wakiwatoza wazazi kujiongezea kipato.
Ripoti hiyo inaonyesha kuwa wazazi wanaoamini kwamba michango hiyo hutumika kulipia ulinzi (asilimia 66) majaribio (asilimia 57) madawati (asilimia 34), mahafali (asilimia nne), na safari za kishule (asilimia nne).
“Ruzuku inayopelekwa moja kwa moja shuleni ambayo ndiyo chanzo kikuu cha fedha kwa shule, inaweza isitoshe kuziba pengo la michango iliyoondolewa,” inasema taarifa hiyo.
Katika ruzuku hiyo, ripoti hiyo inasema sehemu ambayo huelekezwa kwenye vitabu na nyenzo zingine za kujifunzia ni asilimia 40, vifaa vya kuandikia asilimia 20, utawala asilimia 10, na karatasi za mitihani na uchapaji asilimia 10.
Kuhusu ubora wa elimu, asilimia 49 wanasema umeongezeka, asilimia 36 wanasema elimu imezorota na asilimia 14 wanasema hakuna mabadiliko yoyote.
“Asilimia 37 ya wananchi wanaamini kuna uhusiano wa karibu kati ya jitihada za mwalimu na matokeo ya darasa la saba,” ibnabainisha ripoti hiyo.
Kuhusu hadhi ya walimu, wanaoamini kuwa ni msingi wa maendeleo ya nchi ni asilimia 93, wanaheshimika ni asilimia 85, wanajivunia taaluma yao ni asilimia 79, huku asilimia 60 wakiamini walimu wanapewa motisha ya kuhakikisha watoto wanajifunza.
“Pamoja na hayo asilimia 80 ya wananchi wanaamini walimu hufanya kazi yao kwa ajili ya kujipatia kipato,” alisema.