Mgonjwa auza ardhi atoa rushwa 100,000 ili atibiwe

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza daktari kutoka hospitali ya Ligula asimamishwe kazi kwa kosa la kuomba rushwa ya shilingi laki moja ili amfanyie upasuaji mgonjwa.

Waziri mkuu ametoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wauguzi, waganga na wafanyakazi wa hospitali ya mkoa wa Mtwara.

Daktari huyo Fortunatus Nahamala ambaye anafanya kazi ya upasuaji katika hospitali ya Mkoa wa Mtwara Ligula anatuhumiwa kumdai mgonjwa laki moja ili amfanyie upasuaji.

Bi Tatu Abdallah ambaye ndiye amefichua hayo amesema daktari huyo alidai kiasi hicho ili baba yake aweze kufanyiwa upasuaji ndipo baba yake akamruhusu arudi kijijini akauze shamba hekari 2.5 ili zitumike kwenye matibabu.

''Nilimleta baba yangu Februari mosi hapa Daktari aliniambia ninunue dawa za elfu 85,000/= pia ninunue uzi wa kushona kwa shilingi 25,000 pia nimpe daktari 100,000 za kwake lakini hadi Februari 7 baba yangu hakufanyiwa upasuaji'' Amesema Bi Tatu.

Baada ya Bi Tatu kufanya hivyo alimpatia fedha daktari huyo ambaye alimpatia dawa lakini baba yake akakosa huduma hiyo ndipo akaenda kufanyiwa upasuaji hospitali binafsi na kutozwa shilingi elfu 56,000/= ndipo Bi Tatu akaamua kurudisha dawa za daktari huyo ili amrudishie hela zake.