Shule Chalinze zapewa vitabu vya Sh70 milioni


Chalinze. Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete ametoa vitabu vya masomo ya sayansi na hisabati katika shule za msingi na sekondari jimboni humo vyenye thamani ya Sh70 milioni.

Ridhiwani alitoa vitabu hivyo mwishoni mwa wiki iliyopita kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Kulea Childcare Village ili kupunguza tatizo la uhaba wa vitabu vya sayansi.

Akikabidhi vitabu hivyo kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Mdaula, Melkisedek Komba, alisema vitabu hivyo 3,438 vitagawiwa katika tarafa tano zilizopo kwenye Halmashauri ya Mji wa Chalinze.

Alisema Tarafa ya Chalinze itapewa vitabu 998 na nyingine zilizobakia zitapata vitabu 610 kila moja.

Alisema anawatumikia wananchi kwa kutimiza ahadi zake na ataendelea kutatua changamoto za madarasa na madawati katika shule zenye matatizo hayo kadri itakavyowezeka.

Akizungumza kwa niaba ya walimu wakuu wa shule za jimboni humo, Mwalimu Komba alisema msaada huo utasaidia kupunguza tatizo la vitabu lililopo kwenye shule nyingi.

 “Tunashukuru kwa jitihada zako mbunge, ni kweli tulikuwa na uhitaji, lakini sasa tunaomba  Serikali ituongezee walimu wa sayansi , tuna upungufu mkubwa. Kila shule ina upungufu ya walimu wasiopungua watano,” alisema Mwalimu Komba.

Awali, Mwanzilishi wa shirika la Kulea , Romi Mtenda alisema shirika hilo lililoanzishwa mwaka 2007 lina lengo la kusaidia masuala ya jamii, elimu na watoto yatima na wajane.

Alisema kwa Chalinze limeshasaidia dawa katika kituo cha afya cha Chalinze, kujenga matundu ya vyoo kwenye shule za msingi na sekondari.