Wafanyabiashara wa kazi za wasanii waigomea TRA

Mamlaka ya Mapato nchini Tanzania – TRA, imejikuta ikiingia katika mgogoro na wafanyabiashara wanaouza santuri na kazi za wasanii zinazoingizwa kutoka nje na kuuzwa nchini.

Mgogo huo unafuatia zoezi linaloendeshwa na mamlaka hiyo la kukusanya ushuru wa kazi zote za wasanii zinazoingizwa na kuuzwa katika soko la ndani.

Katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam, mamia ya wafanyabiashara wamekusanyika na kulalamikia kufungwa kwa maduka yao, kwa madai kuwa hatua hiyo ni ya uonevu kwani hakuna mfanyabiashara mwenye uwezo wa kwenda kuingia mikataba ya kibiashara na wasanii wa kimataifa na wenye majina makubwa kama ambavyo taratibu za sasa zinavyotaka.

Akijibu madai hayo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA Bw. Richard Kayombo amesema kinachofanywa katika zoezi hilo ni kuitikia agizo la Rais John Magufuli la kuhakikisha mapato yanayotokana na kazi za wasanii yanalindwa.

Kayombo amewataka wafanyabiashara hao kwenda kupata kibali cha haki miliki ya kazi wanazouza kabla TRA haijawapatia stika zitakazoruhusu kazi hizo kuuzwa nchini.