Wamwomba Lukuvi kumaliza utata Kikuyu

Williamu Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaz

WAKAZI wa Kata ya Kikuyu Kusini Manispaa ya Dodoma wamemwomba Williamu Lukuvi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuingilia kati mgogoro wa ardhi unaotokota kwa sasa, anaandika Dany Tibason.

Mmoja wa wakazi hao Asheli Malenda amesema kuwa, wamekuwa wakiishi katika maeneo hayo tangu mwaka 1957 ambapo eneo hilo lilikuwa ni pori lakini hivi sasa wanashanga kuambia si mali yao.

Amesema, awali waliambiwa kuondoka katika eneo hilo na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Mkuu (CDA) kwa madai ya kuwa eneo hilo ni kwa jili ya bustani ya mboga na matunda.

“CDA waliondolewa katika kusimamia eneo hili na kukabidhiwa Manispaa ya Dodoma hali ambayo hivi sasa imekuwa ni kero kwetu kama ilivyokuwa kwa CDA tumeambia hatuna chetu,”amesema.

Mkazi mwingine Sebastina Mkude amesema, tatizo kubwa lipo kwa uongozi wao wa kata “Diwani na mtendaji wetu wote wanamaeneo hapa lakini yao wanadai ni halali na yetu sio. Tunambiwa tuondoke bila kupatiwa malipo yoyote yale,”amesema Mkude.

Juma Mahinda, Mtendaji wa Kata ya Kikuyu amesema, hana kiwanja wala kipande cha ardhi katika maeneo hayo.

Amesema, pamoja na kuwepo kwa mgogoro wa siku nyingi kati ya wanachi na CDA, katika vikao wananchi hao walikubaliana mradi wa upimaji wa ardhi uwe chini ya manispaa.