WBF wasema Cheka alishinda kihalali

Baada Francis Cheka kuibuka na ushindi dhidi ya Geard Ajetovic raia wa Serbia anayefanya kazi zake nchini Uingereza, baadhi ya mashabiki wa michezo nchini wakiwemo wadau wa ngumi wamekuwa na maoni tofauti kuhusiana na matokeo ya mpambano huo.

Mwakilishi wa shirikisho la ngumi za kulipwa duniani nchini Tanzania WBF Yasin Abdalah Ustadhi wakati akitoa ufafanuzi wa kiufundi juu ya ushindi wa Cheka dhidi ya bondia Geard Ajetovic alikuwa akicheza kwa kujihami na kutafuta knock out huku Cheka akipiga ngumi za pointi.

Yassin ametoa ufafanuzi huzi huo kufuatia baadhi ya mashabiki kudai kuwa kuna upendeleo wa matokeo ya pambano hilo.

Ustadhi amesema "Kimchezo kwa mtu aliyetazama mpambano huo katika raundi za mwanzo ambazo Mserbia huyo aliongoza hasa raundi ya kwanza ambayo cheka alidondoka basi atasema moja kwa moja Ajetovic alistahili kushinda huo ni upande wa ushabiki ambao si mtazamo wa kiufundi"

Aidha ustadhi amekwenda mbali zaidi na kutolea mfano mpambano wa dunia kati ya mabondia Mayweather na Pacquiao ambao wengi waliutazama mpambano huo pia kishabiki bila kuzingatia sheria, kanuni na mambo ya kiufundi yanayotawala mchezo huo.

Akiongea zaidi Ustadhi amesema
"Ukiuangalia kwa umakini mpambano huo kiufundi utaona muda mwingi Cheka alionekana kurusha ngumi nyingi kwa mpinzani wake japo nyingi zilionekana nyepesi lakini zilikuwa zikifika sehemu sahihi ya kuzunguka eneo la uso wa mpinzani wake na ndizo zilikuwa zikimpatia alama nyingi tofauti na mpinzani wake ambaye alikuwa akijilinda kwa muda mwingi na kushambulia kwa kushtukiza akivizia ampige Cheka kwa pigo la Knock out kitu ambacho kila muda ulipokuwa ukizidi kusonga ikawa ngumu kwake kutimiza azma hiyo hasa kutokana na Cheka kuzidi kuongeza mashambuliazi kama kawaida yake huku mzungu huyo akionekana kupoteza nguvu"

Akimalizia Ustadhi amewataka mashabiki wa masumbwi hasa wale wasiojua sheria na taratibu za mchezo huo wasipotoshe umma kwa kutoa maneno ya kejeli ama matokeo ya kishabiki bila kuzingatia utaalam wa kiufundi na wao kama WBF wanatangaza rasmi kuwa ushindi wa Cheka ni halali na ulizingatia sheria na uamuzi wa kitaalam na kiufundi.