F DAWASCO YANASA WEZI WA MAJI OYSTERBAY | Muungwana BLOG

DAWASCO YANASA WEZI WA MAJI OYSTERBAY

Bomba la Maji lilounganishiwa kiholela ambalo halina mita linalopeleka huduma ya Maji kwenye jengo kubwa la ghorofa ambalo linamilikiwa na Chuo cha Biashara (CBE) eneo la Oysterbay mtaa wa Msasani Rd Jijini Dar es Salaam.

 Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) limebaini wizi mkubwa wa Maji kwenye eneo la Oysterbey mtaa wa Msasani Rd wakati wa operesheni maalumu yakubaini wezi wa Maji kwenye majengo makubwa Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwenye tukio hilo, Meneja wa Dawasco Kinondoni Bi Judith Singinika alieleza kuwa kwenye operesheni hiyo maalum inayoendelea kutokana na Agizo la Mh. Waziri wa Maji kukagua Majengo yote Makubwa pamoja na viwanda Jijini Dar es Salaam ilikubaini vyanzo vyake vya Maji ,ndipo walipobaini wizi mkubwa wa Maji mtaa wa Msasani Rd kwenye jengo hilo la ghorofa lenye nyumba ndogo(apartments) 25 linalomilikiwa na Chuo cha Biashara (CBE) ambapo kulikutwa na laini mbili zinazoleta Maji na laini moja ikiwa haina mita na ndiyo ilikuwa inafanyiwa Matumizi makubwa.

Pia meneja huyo wa Dawasco ameeleza kuwa wamechukua hatua za kisheria kwa kukitoza chuo hicho faini ya Shilingi milioni 100 ambapo inatakiwakulipwa ndani ya miezi 24 hivyo kila mwezi wanatakiwa kulipa kiasi kisichopungua shilingi milioni 4160000.

“Katika operesheni yetu maalum ya kubaini wezi wa Maji tumeweza kubaini wizi mkubwa wa Maji Oysterbay Kwenye jengo linalomilikiwa na chuo cha biashara (CBE) ambapo wakufuzi wa chuo hicho ndio wanaoishi humo na tumekuta kuna laini mbili zinazoleta Maji moja ina mita na nyingine haina na ndio ina matumizi makubwa hivyo tumewatoza faini na wakubali kuilipa ndani kwa awamu ndani ya miezi 24”, alisema Singinika.

Hata hivyo Dawasco inaendelea kuwasihi wamiliki wote wa Majengo makubwa ya ghorofa pamoja na viwanda waliojiunganishia huduma ya Maji kiholela kijisalimisha kwani operesheni hiyo ni endelevu na hatu kali za kisheria zitachukuliwa kwa yoyote atakaye kamatwa.
Maofisa wa Dawasco Kinondoni waking’oa laini ya Bomba la Maji lilounganishiwa kiholela lisilo na Mita kwenye jengo kubwa la ghorofa linalomilikiwa na Chuo cha Biashara (CBE) eneo la Oysterbay mtaa wa Msasani Rd Jijini Dar es Salaam.