Elimu juu ya uzalishaji wa mbegu za mpunga

Mbegu ndio msingi wa kiumbe hai chochote. Mbegu za mazao kama mpunga hutunza sifa za kijenetiki za mmea hivyo matumizi ya pembejeo zingine za kilimo ni katika tu kusaidia mbegu iweze kutoa mavuno kwa kiwango kinachotegemewa. Ndio maana pembejeo zingine kama mbolea zisipotumika mbegu huweza kutoa mavuno kidogo tu lakini pembejeo zingine hizi haziwezi kutumika bila mbegu.

1. Umuhimu na kanuni za mbegu bora.
a. Kwanini mbegu bora?
Mbegu bora za mpunga zimetafitiwa ili kukidhi mahitaji ya wadau muhimu katika sekta ya mpunga kama vile:

i. Wakulima --- Mavuno mengi
ii. Wasindikaji --- Ukobolekaji
iii. Wafanyabiashara --- Mwonekano k.m. punje ndefu na nyembamba
iv. Walaji --- Radha, kupikika,


b. Faida za kutumia mbegu bora

  • Zimetiwa dawa ya kuzuia magojwa ya udongoni, vijidudu na fangasi hivyo kuiepusha mbegu na mche kutokana na mashambulio ya magonjwa, wadudu na fangasi.
  • Zina uotaji wa kiwango cha juu hivyo huokoa gharama ya mbegu. TOSCI hudhibitisha mbegu ya mpunga ikiwa tu uotaji wake ni zaidi ya 80%.
  • Huokoa gharama


Mfano:
Jedwali la matumizi ya mbegu katika Ekari moja na gharama zake
Mbegu
Kiasi cha mbegu kwa Ekari
Gharama ya mbegu
Jumla ya gharama ya mbegu
Mbegu bora iliyothibitishwa
Kilo 4 hadi 8
TSH 3,000 kwa kilo
12,000 hadi 24,000
Mbegu isiyo bora
Debe 2 hadi 3
TSH 10,000 kwa debe
20,000 hadi 30,000


c.    Mbegu bora
  1. Ni halisi (genetic pure)
  2. Ni safi, haina mchanga, mapepe wala masuke
  3. Viwango vya uotaji viko juu
  4. Hutoa mimea yenye afya njema
  5. Huvumilia baadhi ya magonjwa na wadudu
  6. Hukomaa pamoja
  7. Mchele wake huiva kwa pamoja ukipikwa

2.    Uzalishaji wa mbegu bora
a.    Uchaguzi wa shamba na maandalizi kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu
Sifa za shamba
i.  Tambarare, lisilo na miinuko 
ii.  Lisilo na mafuriko 
iii. Lisilo na vivuli 
iv.  Kuingiza maji na kuyatoa kiurahisi (good drainage)
b.  Kukokotoa Kiasi cha mbegu
Kiasi cha mbegu = mbegu inayotakiwa kwa ekari x eneo (ekari)
                                                                  Uotaji (%)
c.    Utenganisho wa shamba la mbegu ya na mashamba mengine ya mpunga
Uchavushaji waweza kusababishwa na:
  • Upepo 
  • Wadudu
  • Ndege
  • Konokono
  • Maji
Shamba la mbegu ya mpunga iliyothibitishwa litengane na mengine kwa mita 

d.Uthibiti magugu
  • Magugu hupunguza wingi na  ubora wa mbegu
  • Shamba liwe safi muda wote
  • Sheria mbegu imekataza aina fulani ya magugu kutokuwepo kabisa shambani k.m bhangi, mpunga pori, kiduha

e.Kuondoa mimea isoyo mbegu (off-type)
Mfano wa off-type
  1. Mimea ya mpunga iliyojiotea yenyewe mathalan kutoka msimu uliopita 
  2. Kubadilika kwa sifa za kijenetiki za mmea 
  3. Mchanganyiko wa mbegu kwa bahati mbaya
  4. Utambuzi wa off-type
  5. Mimea mifupi ama mirefu zaidi ya wenzao shambani 
  6. Mimea yenye rangi tofauti za majani, masuke 
  7. Mkia wa punje (awn) 
  8. Mimea inayowahi zaidi ama kuchelewa zaidi kuchanua (mimea itofautiane kati ya siku 2-3) 
  9. Mkao wa jani la juu katika suke (lag leaf angle) 
  10. Ukubwa, umbo na rangi ya punje 
  11. Mimea iliyoshambuliwa na ugonjwa/wadudu
  12. Kuondoa maotea (off-type) kufanyike angalau mara moja wakati wa:
  13. hatua ya ukuaji wa majani (vegetative growth) 
  14. kuchanua 
  15. baada ya kuchanua 
  16. kabla ya kuvuna

f. Udhibiti wa wadudu na magonjwa shambani 
Ifahamike kwamba, wadudu na magonjwa huathiri wingi na ubora wa mbegu ya mpunga hasa viwapo shambani.


g. Matumizi ya mbolea
Matumizi sahihi ya mbolea huongeza ubora na wingi wa mavuno ya mbegu ya mpunga.


3. Uvunaji na huduma baada ya kuvuna mbegu bora
a. Muda wa kuvuna (Timing)
Kuwahi ama kuchelewa hupunguza ubora na mavuno
Athari ya Kuwahi kuvuna
  • Mbegu zisizojaza vizuri 
  • Mavuno/ubora kidogo 
  • Kupoteza uotaji
  • Athari za Kuchelewa kuvuna 
  • Mashambulizi ya wadudu, ndege 
  • Kuanguka 
  • Kupukutika
  • Muda sahihi wa kuvuna
  • Punje hugeuka kuwa njano-kahawia 
  • 80% ya majani imebadili rangi kutoka kijani na kuwa rangi ya mabua 
  • Unyevu wa punje 20-22% 
  • Punje huwa ngumu na hazivunjiki kirahisi zikitafunwa

b.    Kukausha mbegu ya mpunga
Mbegu yenye unyevu kidogo huweza kutunzwa kwa kipindi kirefu bila kuharibika (kuvuna, kupoteza uotaji).

Unyevu wa mbegu
Muda wa kudumu gharani
14-18%
Wiki 2 -3 tu
13%
Miezi 8-12
9%
Zaidi ya mwaka


4. Viwango vya mbegu
Mbegu bora huzalishwa kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu hivyo vimewekwa viwango ambavyo ili mbegu ithibithishwe ni lazima vifikiwe.
Vipo viwango vya shambani na maabara kama ifuatavyo:

a. Viwango vya shambani

Kigezo
Kiwango
Shamba (misimu kabla)
2
Utenganisho
mita 5 na zaidi
Awamu za ukaguzi
2 na zaidi
Maotea (off-types)
0.1
Mazao mengine
0.05%
Magugu yaliyozuiwa
0
Mimea ya Mpunga pori
0.1%

                             
b.    Viwango vya maabara
Kigezo
Kiwango
Mbegu halisi (Pure Seed)
98.0% na zaidi
Mbegu zingine (Other Seed)
0.1 na pungufu
Makapi (masuke, vijiti, majani)
1.9% na pungufu
Unyevu wa mbegu
13.0% na pungufu
Uotaji
80% na zaidi
Mbegu za magugu yaliyozuiliwa
0.0%
Mbegu za magugu yayokatazwa
punje 4 kwa kilo na pungufu

Baadhi ya Magugu yaliyozuiliwa
  • Kiduha/Magugu chawi (sani)
  • Bangi
  • Kokeini

Magugu yaliyokatazwa
  • Ndago
  • Mpungapori
  • Mashikanguo