Aliyegombea urais CCM aomba kazi kwa JPM

Aliyekuwa mtiania wa kugombea nafasi ya urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Siyantemi, amemtaka Rais John Magufuli kumpa kazi ili amsaidie kurejesha nidhamu ya wafanyakazi na kuongeza mapato ya Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Siyantemi alisema kazi nyingi anazozifanya Rais Magufuli alitarajia kuzifanya hata yeye kama angepewa ridhaa hiyo.

“Nataka ni mwambie Rais hayupo peke yake kwenye jitihada hizi, bali tupo vijana shupavu na wazalendo kwa nchi yetu na hata nilipokuwa nikinadi sera zangu wakati ule nagombea, nilisema nitapiga vita rushwa kwa sababu ni ugonjwa mbaya unaoiangamiza jamii,” alisema Siyantemi.

Alisema anatamani kufanya na kazi Dk Magufuli kwa sababu anazisimamia hoja ambazo hata yeye alizizungumzia wakati wa kutangaza nia.

Siyantemi alisema Watanzania wana imani na Dk Magufuli kwa kuwa anadhibiti suala la watumishi hewa, uingiaji mikataba mibovu, kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kudhibiti ukwepaji kodi, kuziba mianya ya upotevu wa fedha za umma na kuhimiza nidhamu ya matumizi ya fedha za Serikali.

“Kuna vibaraka wachache wasioitakia mema nchi ambao pia wanajaribu kumkatisha tamaa rais na wamekuwa wakishirikiana na mabeberu kutoka nje ya nchi…Tunapaswa kutambua nchi haitaendelea kwa misaada na fedha za wafadhili wa nje, bali ni kwa juhudi zetu,” alisema.

Alisema Watanzania wanakabiliwa na changamoto nyingi za kijamii na kiuchumi na kushauri kuanzishwa kwa utaratibu wa kila Mtanzania mwenye kipato kuchangia Sh1,000 kwa mwezi kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Alisema ataendelea kushiriki katika jitihada za kupambana na rushwa na ufisadi na kwamba, wale wote watakaothibitika kuhusika na rushwa watajwe hadharani na kufilisiwa mali zao.