Majaliwa: Tutaufanyia kazi ushauri wa Zitto

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeupokea na itaufanyia kazi ushauri wa Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe aliyetaka Benki ya Standard ICBC ya Uingereza na kampuni dada ya Stanbic Tanzania kuchunguzwa juu ya mkopo wa hatifungani wa Sh1.2 trilioni ambao umegubikwa na ufisadi.

Zitto alitoa kauli hiyo juzi wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais-Tamisemi na Utawala Bora mwaka 2016/17 na kutaka Bunge liunde kamati teule kuchunguza suala hilo na ukweli ukibainika, Serikali itakwepa kulipa deni la Sh2 trilioni ambazo Tanzania inatakiwa kulipa ikiwa ni deni na riba.

Majaliwa alitoa kauli hiyo jana mjini Dodoma baada ya kuulizwa swali na waandishi wa habari juu na hatua ambazo Serikali imezichukua kutokana na sakata hilo linalodaiwa kuwa na harufu ya ufisadi, kwamba baada ya uchunguzi kukamilika taarifa itatolewa.

“Nikiwa kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni nimeupokea ushauri wake na kwa kweli tutaufanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuchunguza,” alisema Majaliwa.

Wakati akichangia mjadala huo, Zitto alisema Machi 2013, Serikali ilikopa Sh1.2 trilioni kwa msaada wa Benki ya Standard ya Uingereza, ambayo kwa sasa inaitwa Standard Bank ICIC plc na kwamba mkopo huo umeanza kulipwa Machi mwaka huu mpaka mwaka 2020 kwa mikupuo tisa.

Alisema mpaka kufika mwaka 2020 Tanzania italipa deni pamoja na riba ya Sh2 trilioni huku kukiwa na wasiwasi kwamba fedha ambazo zilipatikana kutokana na mkopo huo hazikufika kule kunakotakiwa.

“Nimewasilisha taarifa zangu wizara ya fedha na mipango kutaka kujua miradi ambayo fedha hizi zilikwenda ingawa kwa orodha ya miradi aliyonayo na kutokana na habari za hivi karibuni za Serikali kudaiwa na makandarasi, miradi ya Kinyerezi na Kiwira, inaonyesha sehemu ya fedha zilizopatikana katika mkopo huu hazikupelekwa huko,” alisema Zitto.

“Jambo la kushangaza ni kwamba wanaosemekana kula rushwa hiyo hawapo mahakamani mpaka sasa. Vilevile waliotoa rushwa hiyo hawapo mahakamani mpaka sasa. Waliopo mahakamani ni wanaosemekena kutumika kupeleka rushwa,” alisema.

“Mjumbe kashtakiwa, lakini aliyemtuma hajashtakiwa na aliyepelekewa kilichotumwa hajashtakiwa. Hapa kuna tatizo la msingi ambalo tukilitatua Serikali yetu itaepuka masuala kama haya siku za usoni.”

Alisema ana barua ya kundi la Watanzania zaidi ya 2,000 wakitaka benki hiyo ya Uingereza ichunguzwe katika suala hilo la hati fungani huku Takukuru wakitumia taarifa ya Taasisi ya Uingereza ya (SFO) katika kuchukua hatua zinazostahili dhidi ya Watanzania wanaotajwa katika sakata hilo.

Alisema SFO haikufanya uchunguzi dhidi ya benki hiyo ya Uingereza na kushangazwa na Tanzania kusaidiwa kesi hiyo na wataalamu kutoka nchi hiyo.

“Iwapo tutafanikiwa kuonyesha kuwa benki ya Standard ilihonga kupata biashara nchini kwetu, Tanzania itakuwa fundisho kwa kampuni ya kimataifa kwamba Afrika si mahala pa kuhonga na Tanzania haitalipa mkopo huu na riba zake na tutaokoa zaidi ya Sh2 trilioni katika deni la Taifa,” alisema.

Wakati huohuo, Rais John Magufuli jana alikutana na maofisa wakuu wa Jeshi la Polisi mjini Dodoma katika kikao kilichofanyika katika ukumbi mpya wa CCM.

Taarifa zinaeleza katika kikao hicho ambacho waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuhudhuria, Rais aliwakumbusha maofisa hao majukumu yao ya kazi na kupanga mikakati mbalimbali.