Polisi wamshikilia mwanachuo kwa wizi benki

Jeshi la Polisi linamshikilia mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro kwa tuhuma za kutumia kadi ya kutolea fedha benki (ATM) ya mwanafunzi mwenzake na kufanikiwa kutoa kiasi cha Sh500,000 katika tawi la CRDB Masika mjini hapa.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Ulrich Matei alimtaja mtuhumiwa kuwa ni Saada Saidi (23) akidai kwamba alitenda kosa hilo Aprili 23 saa nne asubuhi.

Kamanda Matei alidai kuwa mtuhumiwa huyo alichukua kadi ya benki ya rafiki yake, Zainab Adinani na kwenda nayo benki kwa lengo la kutenda uhalifu. Alisema wanafunzi hao wako mwaka wa tatu wakisomea Shahada ya Ualimu.

Kamanda Matei alidai kwamba siku ya tukio mtuhumiwa alimuaga rafiki yake kwamba anafika mjini mara moja. Baada ya mtuhumiwa kufanikiwa kutoa fedha kwa kadi hiyo, mmiliki halali wa kadi, Zainab, alipokea ujumbe mfupi kupitia simu yake ya mkononi ukimtaarifu kuwa kuna fedha zinatolewa kwenye kadi yako kama huna habari toa taarifa ndipo alipoaanza kufuatilia.

Kamanda alidai kuwa walipowahoji waligundua kwamba baaada ya mtuhumiwa kurejea wanapoishi alimkuta rafiki yake akitafuta kadi yake na walisaidiana kutafuta bila mafanikio na ndipo walipoamua kufika CRDB tawi la Masika kwa msaada zaidi.