TFF yawaruka wazee Yanga

Homa ya mechi tano za mwisho za Ligi Kuu impanda na kuiumiza Yanga kiasi cha kuwalazimisha wazee wa klabu hiyo kulitaka Baraza la Michezo Tanzania (BMT) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusogeza mbele mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo unaoanza Mei 3.

Wazee hao wanataka mchakato huo usubiri ligi imalizike, jambo ambalo TFF ilijibu jana kuwa haishughuliki na wazee, bali Yanga kama mwanachama wake.

Ofisa habari wa TFF, Alfred Lucas alisema jana shirikisho hilo haliwezi kufanyia uamuzi mambo yaliyozungumzwa na wanachama, bali uongozi wa klabu hiyo unafahamu taratibu za kuwasiliana na shirikisho hilo.

“Kwanza, maombi ya kutaka kusogezwa kwa mchakato wa uchaguzi hatujayapata, lakini hao waliozungumza ni wanachama, na sisi, TFF huwa tunafanya kazi na wanachama wetu na miongoni mwao ni klabu ikiwamo Yanga.

“Hivyo, tunafanya kazi na uongozi wa Yanga na siyo wanachama wa Yanga, sasa uongozi wa Yanga unafamu taratibu za kufuata ili kuwasiliana na TFF,” alisema Lucas.

Kwa upande wake, katibu mkuu wa BMT, Mohammed Kiganja alisema hawezi kujibu chochote kwa sababu Yanga hawajapeleka barua ya maombi hayo pia hata kama wakipeleka inabidi waende kwanza TFF.

Mwezi huu, BMT iliiagiza TFF ihakikishe Yanga inaanza mchakato wake wa uchaguzi haraka na kuhakikisha inafanya uchaguzi kabla ya Juni 30 kwa sababu haiwatambui viongozi waliopo madarakani wanaoongozwa na mwenyekiti, Yusuph Manji.

Kutokana na agizo hilo, TFF kupitia kwa mwenyekiti wake wa kamati ya uchaguzi, Wakili Aloyce Komba alitangaza kuwa uchaguzi mkuu wa Yanga utafanyika Juni 5 na mchakato wa uchaguzi huo utaanza Mei 3 huku Mei 4 hadi 9 ikiwa ni siku ya wagombea kuchukua fomu na kurudisha.

Mapema jana wazee wa klabu hiyo waliibuka na kueleza kuwa wamefikiria na kuona kuwa endapo mchakato huo utaanza wiki ijayo utawavuruga katika harakati zao za kuhakikisha timu yao inatwaa ubingwa.

Mwenyekiti wa wazee hao, Ibrahim Akilimali aliiomba BMT na TFF kusogeza mbele mchakato wa uchaguzi mkuu hadi baada ya kumalizika kwa ligi, Mei 21.

Alisema kuanza kwa mchakato wa uchaguzi wakati timu ikikabiliwa na michezo mitano migumu ugenini tena ikiwa bingwa mtetezi kunaweza kukaivuruga kwa sababu kila mwanachama ana mgombea wake hivyo yanaweza kuibuka mengine.

“Sisi tunaheshimu vyombo vyote vinavyosimamia soka, tunapenda kushirikiana navyo kwa manufaa ya Yanga na michezo kwa jumla, hivyo tunaiomba BMT na TFF kusogeza mbele mchakato wa kuanza kuchukua fomu na taratibu zake na uanze baada ya kumalizika kwa ligi. “Hivi sasa ligi inaelekea ukingoni, tupo kwenye vita ya kutetea ubingwa, tuna fainali ya FA, pia tuna mashindano ya kimataifa, hivyo kwa hatua ya sasa tuliyofikia kwenye ligi tunahitaji mshikamano na umoja.” alisema.