Urusi na Marekani zalaumiana kuhusu uchokozi wa ndege

Urusi inasema kuwa ilikuwa na haki kuikabili ndege moja ya Marekani katika bahari ya Baltic siku ya Ijumaa.

Hatua hiyo inajiri baada ya Marekani kusema kuwa ndege ya kijeshi ya Urusi ilizua hofu ya kiusalama baada ya kuzunguka karibu na ndege yake.

Urusi inasema kuwa ndege hiyo ya Marekani ilikuwa imezima kifaa chake cha kurusha ishara zake ambazo husaidia wengine kuitambua.

Ni kisa cha pili katika bahari ya Baltic mwezi huu ambapo Marekani imezishtumu ndege za Urusi kwa kupaa kwa uchokozi.

''Ndege zetu zote za Urusi zinafuata sheria za kimataifa kuhusu utumiaji wa anga'',taarifa ya wizara ya Ulinzi nchini Urusi ilisema.

''Ndege za Marekani zina mambo mawili:Zisiruke karibu na mpaka wetu ama ziwashe ishara ili kutambulika''.

Ndege za Marekani mara kwa mara hujaribu kupaa karibu na anga ya Urusi bila taa zinazoonyesha ishara taarifa hiyo ilisema.

Katika kipindi cha miezi 18 iliopita,Urusi pia imeshtumiwa kwa kutekeleza kitendo kama hicho katika bahari ya baltic pamoja na karibu na maji ya Uingereza.