Apoteza fahamu baada kuhukumiwa kifungo cha maisha

Dar es Salaam. Mkazi wa Karakata mpya jijini Dar es Salaam, Athuman Rajabu  (19) ameanguka na kupoteza fahamu  katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti na kumbaka mfanyakazi wake wa ndani wa miaka 13.

Kutokana na hali hiyo, mahakama ilisimamisha shughuli zake kwa muda hadi alipozinduka.

Akisoma hukumu hiyo leo, hakimu Saidi Mkasiwa amesema mahakama imemtia hatiani mshtakiwa huyo baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi watano waliotoa ushahidi wao dhidi ya mshtakiwa.

“Mshtakiwa atatumikia kifungo cha maisha jela baada ya mahakama yangu kuridhishwa na ushahidi wa mashahidi watano wa upande wa mashtaka waliotoa dhidi yake na ili iwe fundisho kwa vijana wengine wenye tabia mbaya kama hizi,” amesema.

Kabla ya hukumu, upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Sylvia Mitando aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo.

“Mheshimiwa hakimu naiomba mahakama yako kutoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyu kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo,” amesema wakili Mitanto.

Mshtakiwa alitenda kosa hilo kati ya Oktoba na Novemba mwaka 2014, katika eneo la Karakata mpya Wilaya ya Ilala.

Katika shtaka la kwanza mshtakiwa amembaka mtoto wa miaka 13 huku shtaka la pili akimlawiti mtoto huyo ambaye alikuwa mfanyakazi wake wa ndani.

Katika ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, imedaiwa kuwa mshtakiwa huyo alikuwa anakaa chumba kimoja na mkewe, mtoto wake na mfanyakazi huyo.

Inadawa kuwa Rajabu alikuwa akimfanyia vitendo hivyo mfanyakazi huyo wa ndani wakati mkewe alipokuwa akienda kazini asubuhi.