Mwalimu kortini akidaiwa kughushi vyeti

Dar es Salaam. Mwalimu wa Shule ya Msingi Kisutu, Marth Komanya amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kujibu mashtaka manne yanayomkabili likiwamo la kugushi cheti cha ualimu.

Mshtakiwa amefikishwa mahakamani hapo leo na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Catherine Kiyoja.

Wakili wa Serikali, Grace Mwanga amedai mahakamani hapo kuwa  siku zisizojulikana mshtakiwa alighushi cheti chenye namba S. 375\55 ambacho kilionyesha amemaliza elimu ya sekondari wakati akijua kuwa siyo kweli.

Shtaka la pili, mwalimu huyo amedaiwa kuwasilisha nyaraka katika Manispaa ya Ilala ambazo zilikuwa zinaonyesha amemaliza elimu ya sekondari wakati akijua siyo kweli.

Mwanga amedai katika shtaka la tatu na nne kuwa mshtakiwa amegushi cheti cha ualimu chenye namba 71844 kikionyesha alipata daraja la 3A na kuwasilisha katika Manispaa ya Ilala, wakati akijua kuwa ni uongo.

Mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yanayomkabili alikana kutenda makosa hayo.

Hakimu Kiyoja ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 13, mwaka huu itakapotajwa tena.

Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili ambao ni wafanyakazi kutoka taasisi inayotambulika kisheria waliosaini bondi ya Sh2 milioni kila mmoja.