SEKTARIETI YA AJIRA YANATOA RAI KWA WAOMBAJI FURSA ZA AJIRA KUJISAJILI KATIKA MFUMO WA AJIRA.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Raisi Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma, Riziki Abraham akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya sektarieti ya ajira inatoa rai kwa waombaji fursa za ajira kujisajili katika mfumo wa ajira unaopatikana kupitia anuani portal.ajira.go.tz na mfumo wa “job alert system” kwa kubofya  *152*00# ili kuweza kuomba fursa za ajira zinapopatikana,  leo jijini Dar es Salaam kulia ni Kaimu Naibu Katibu wa Tehama Mage Ugullum.

Waandishi wa habari wakimsikiliza Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Raisi Sekretarieti ya Ajira Katika Utumishi wa Umma, Riziki Abraham jijini Dar es Salaam.

SEKRETARIETI ya Ajira katika Utumishi wa Umma ambayo imepewa dhamana ya kuendesha mchakato wa Ajira kwa niaba ya waajiri mbalimbali Serikalini, imeboresha na kurahisisha mchakato wa Ajira kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA katika kutangaza nafasi za kazi, kupokea maombi, kuwaita kwenye usaili na kuwapa wadau taarifa mbalimbali za kazi pamoja na kuwawezesha waombaji kazi kutumia teknolojia kupata Ajira.

Akizungumza na waandishi wa habari Msemaji wa Sekretarieti hiyo Bibi Riziki Abraham amesema kuwa katika kuwawezesha wananchi hususan waombaji fursa za Ajira kupata taarifa za Ajira kwa wakati na uhakika, Sekretarieti ya Ajira pamoja na kutumia tovuti yake ya www.ajira.go.tz imeanzisha mifumo mingine miwili ya kielekroniki ili kuhakikisha kuwa maombi yote ya fursa za Ajira yanapokelewa  na taarifa mbalimbali kuhusu Ajira zinawafikia Watanzania wengi zaidi hususan wanaoishi vijijini na nje ya mipaka ya nchi yetu.

Amebainisha mifumo hiyo kuwa ni pamoja mfumo wa kuomba fursa za Ajira unaojulikana kama “recruitment portal” na unapatikana kwa anuani “portal.ajira.go.tz” na mfumo wa pili ni kwa ajili ya kupata ujumbe mfupi wa fursa za Ajira za papo kwa papo kupitia simu za kiganjani ujulikanao kama “Job alert system” na unaweza kuupata kwa kubofya *152*00# na kufuata maelekezo.

Akizungumzia sababu za kuanzishwa kwa mfumo huo Bibi Riziki amesema kuwa mifumo hiyo inalenga kupunguza changamoto kadhaa zikiwemo  Malalamiko ya baadhi ya waombaji fursa za Ajira kuhusu upotevu wa maombi yao ya kazi, Mchakato wa Ajira kuchukua siku nyingi ili kukamilika (Takribani siku 90 kukamilisha mchakato wa Ajira), Namna ya kuzihifadhi taarifa zote za waombaji fursa za Ajira na kazi ya rejea pale kunapokuwa na haja ya kufanya hivyo, Kupunguza gharama za kuendesha mchakato wa Ajira na mwisho ni kuhakikisha tunapanua wigo wa utoaji taarifa za uwepo wa fursa za Ajira hasa kwa waombaji fursa za Ajira waishio vijijini.

Kwa upande wake kaimu Naibu katibu wa TEHAMA katika Sekretarieti hiyo Bibi Mtage Ugullum ameongeza kuwa tangu kuanza mfumo wa utumaji maombi ya kazi kwa njia ya kieletroniki (recruitment portal) kumekuwa na manufaa makubwa ambapo umeweza kupunguza muda wa uendeshaji wa mchakato wa Ajira kutoka siku 90 hadi siku 52 kwa sasa. Pia mfumo huu umesaidia waombaji wa kazi kuwa na uhakika wa maombi yao kupokelewa kwa wakati na kupata mrejesho wa papo tofauti na ilivyokuwa zamani ambapo maombi ya kazi yalikuwa yakipokelewa.

Ameongeza kuwa mfumo wa “Job alert” kwa kutumia simu za kiganjani umeongeza idadi kubwa ya waombaji wa fursa za Ajira na umerahisisha taarifa za fursa za Ajira kufika maeneo mengi zaidi, kwa kuwa kinachotakiwa ni mhusika kuwa na simu na kujisajili katika mfumo atapata taarifa za kazi zilizotangazwa na Serikali wakati huo.

Hadi kufikia tarehe 29 Mei, 2016, jumla ya waombaji wa fursa za Ajira waliojiandikisha kwenye mfumo wa utumaji maombi ya kazi walikuwa (97,765). Aidha, jumla ya waombaji wa fursa za Ajira (89,484) wamejiunga kwenye mfumo wa kupata taarifa za uwepo wa fursa za Ajira kupitia simu za kiganjani na barua pepe.

Sekretarieti ya Ajira inatoa Rai kwa waombaji fursa za Ajira wakiwemo wanafunzi wa Vyuo vikuu wanaotaraji kuhitimu hivi karibuni kujisajili katika mfumo wa Ajira unaopatikana kupitia anuani portal.ajira.go.tz na mfumo wa “Job alert system” kwa kubofya *152*00# ili kuweza kuomba fursa za ajira zinapopatikana.