TPDC KUSHIRIKIANA NA KAMPUNI YA KITANZANIA

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio (kushoto) na Mkurugenzi wa Minjingu, Bw. Pardeep Hans wakipeana mikono mara baada ya kutiliana sahihi Mkataba wa Makubaliano (MoU) katika utafiti wa mafuta na gesi na kufanya tathimini za kina katika Kitalu cha Songo Songo Magharibi.

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya MINJINGU Mines & Fertliser Ltd ya Arusha wametia sahihi Hati ya Makubaliano (MoU) kushirikiana katika kufanya tathimini za kina katika kitalu cha Songo Songo Magharibi.

Akiongea baada ya kutia sahihi hati hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt. James Mataragio alisema makubaliano kati ya TPDC na Kampuni ya Minjingu yanafungua fursa ya kufanya tathmini za kitaalamu kwa pamoja juu ya takwimu zilizopo za kitalu cha Songo Songo Magharibi ambacho kinamilikiwa na TPDC nia ikiwa ni kutafuta mashapo ambayo yanaweza kuhifadhi mafuta au gesi asilia.

“TPDC tayari ina takwimu nyingi kuhusu Kitalu cha Songo Songo Magharibi na itafanya kazi kwa karibu na Kampuni ya MINJINGU kuhakikisha kunakua na mafanikio katika mradi huu” amesema Dkt Mataragio.

Dkt. Mataragio amesisistiza kuwa makubaliano hayo yanatoa wajibu kwa pande zote mbili kufanya kazi kwa pamoja ndani ya kipindi cha mwaka mmoja kutathmini uwezekano wa mashapo ya kitalu cha Songo Songo Magharibi kuhifadhi mafuta au gesi.

“Iwapo kutakua na matokeo chanya basi hatua zingine za utafiti ikiwemo kuchimba kisima zitafuata” aliongezea Dkt. Mataragio.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Minjingu, Ndugu Pardeep Hans alisema wao kama kampuni ya kizawa wamefurahi sana kuaminiwa na Serikali na watafanya kazi kwa weledi wa hali ya juu wa kushirikiana na TPDC ili kuhakikisha wanafikia lengo la ushirikiano wao.

“Endapo gesi itagundulika basi itatumika kutumika katika mradi wa mbolea ambao MINJINGU wako ubia na TPDC” pamoja na Ferrostaal kutoka Ujerumani, Haldor Topsoe ya Denmark na Fauji ya Pakistani” alisema Bw. Hans.

Makubaliano hayo ya awalia yanafungua fursa ya TPDC pamoja na MINJINGU ya ushirikiano wa utafiti katika Kitalu cha Songo Songo Magharibi, Kampuni ya Mijingu ikiwa Kampuni ya kwanza ya Kizawa kushirikiaa na TPDC katika utafiti wa mafuta na gesi.