Ulimwengu kambini na Taifa Stars kuivaa Misri

Nyota wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu amejiunga na timu ya taifa, Taifa Stars leo kwa ajili ya mchezo wa kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika dhidi ya Misri Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ulimwengu amechelewa kujiunga na Taifa Stars kutokana na klabu yake, TP Mazembe ya DRC Congo kumuomba abaki kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu nchi humo. Mchezaji huyo ameingia nchini leo, jijini Dar es salaam na moja kwa moja kuingia kambini.

Taifa Stars sasa inamsubiri mshambuliaji na Nahodha, Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji pekee, ambaye naye klabu yake ilimuomba abaki kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa mchujo wa kuwania kucheza Europa League msimu ujao.

Samatta na Ulimwengu, wote wameziongoza klabu zao kushinda mwishoni mwa wiki, Genk ikiilaza 5-1 Sporting Charleroi na kufuzu Europa League na Mazembe ikiichapa 2-0 AS Vita katika Ligi ya DRC Congo.